Kimataifa

WABEBA SILAHA WAVAMIA SHULE NA KUTEKA NYARA WATOTO 225 NIGERIA

Wasichana waliotekwa wakisubiri kuungana na familia zao katika jimbo la Zamfara Machi 3 2021. Picha na Aminu ABUBAKAR / AFP.

Wanafunzi katika shule ya msingi jimboni Kaduna.

****************************************

Watu wenye silaha wameshambulia shule na kuwateka nyara watoto zaidi ya 200 huko kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Mwalimu wa shule hiyo Sani Abdullahi katika mji wa Kuriga jimboni Kaduna ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa takwimu walizochukua pamoja na wazazi zinaonesha kuwa, idadi ya wanafunzi wa sekondari waliotekwa nyara ni 187, na 40 wa msingi.

Diwani katika mji wa Kuriga, Idris Maiallura amesema awali kundi hilo la wabeba silaha lilikuwa limewateka nyara wanafunzi 100 wa shule ya msingi lakini baadaye likawaachia huru kadhaa miongoni mwao.

Naye Gavana wa Kaduna, Uba Sani amelitembelea eneo la tukio na kuahidi kuwa wanafunzi hao waliotekwa nyara wataachiwa huru na kwamba operesheni ya kuwakomboa inaendelea. 

Shambulio hilo la utekaji nyara linahesabika kuwa kubwa zaidi tangu mwaka 2021, na pia tangu Rais Bola Ahmed Tinubu aingie madarakani, na kuahidi kukabiliana na changamoto za usalama nchini humo.

Kaduna ni mojawapo ya majimbo kadhaa ya kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria yanayotishwa na majambazi wanaovamia vijiji, kuua na kuwateka nyara wakazi pamoja na kuchoma nyumba baada ya uporaji. Magenge hayo yana kambi katika msitu mkubwa unaozunguka majimbo ya Zamfara, Katsina, Kaduna na Niger.

Mnamo Februari 2021, majambazi walivamia shule ya bweni ya wasichana katika mji wa Jangebe katika jimbo la Zamfara, na kuwateka nyara zaidi ya wanafunzi 300. Wasichana hao waliachiliwa siku chache baadaye kufuatia malipo ya fidia ambayo ililipwa na serikali.

Nigeria inakabiliwa na changamoto lukuki za kiusalama, ikiwa ni pamoja na hujuma za muongo mmoja na nusu za magaidi wakufurishaji wa Boko Haram kaskazini mashariki ambao wameua takriban watu 40,000 na kuwalazimisha wengine zaidi ya milioni mbili kukimbia makazi yao.

About the author

mzalendo