Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Tuggar amesema nchi yake inajipanga kuomba uanachama katika jumuiya ya kiuchumi ya BRICS baada ya mipango muhimu ya uratibu wa ndani ya nchi hiyo kukamilika.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Nigeria ambaye wiki hii alikuwa mjini Moscow, Russia kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Machi 5 hadi 7 amekutana na mwenyeji wake Sergey Lavrov na kujadili uhusiano wa nchi hizo mbili, pamoja na ajenda za kikanda na kimataifa.
Tuggar amefanyiwa mahojiano pia na shirika la habari la Sputnik na kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwezekano wa Nigeria kuwa mwanachama wa BRICS na akasema, “tunakusudia kufanya hivyo.
“Kama nilivyosema hapo awali, Nigeria inaendesha mfumo wa kidemokrasia wa majadiliano na mashauriano. Kwa hivyo inapasa kufanya mazungumzo na majadiliano mengi na makundi tofauti ya masilahi na vyombo tofauti vya ndani kabla ya hatua kama hiyo kuchukuliwa”,amesema.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria ameashiria umuhimu wa kushiriki Makamu wa Rais wa nchi hiyo Kashim Shettima katika Mkutano wa 2023 wa BRICS nchini Afrika Kusini na kusisitiza kwamba nchi yake ina hamu ya suala hilo na ina matarajio ya kulifikia.
Mnamo Novemba 2023, Tuggar alifichua kuwa Nigeria itaomba kujiunga na BRICS ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo ili kufanikisha uwakilishi na ushawishi wa taifa hilo katika jukwaa la kimataifa. Pia alisema, taifa hilo la Afrika Magharibi liko tayari kujiunga na muungano wowote ambao una malengo ya ujengaji na yaliyoainishwa vyema.
Kundi la BRICS la nchi zinazoinukia kiuchumi, ambalo hadi hivi karibuni lilikuwa na wanachama wake wakuu watano tu, ambao ni Brazil, Russia, India, China, na Afrika Kusini, limepata upanuzi mkubwa Januari mwaka huu wakati Iran, Ethiopia, Misri na Muungano wa Falme za Kiarabu zilipojiunga nalo Saudi Arabia pia imealikwa na iko tayari kuwa mwanachama. Mataifa mengine mengi yameonyesha nia ya kujiunga huku mengine yakiwa tayari yameshatuma maombi rasmi.