Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, akizungumza Machi 7,2024 jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa ushirikiano na Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani Machi 08.2024
Baadhi ya Washiriki wakimsikiliza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (hayupo pichani), wakati akifungua Kongamano la wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa ushirikiano na Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani Machi 08.2024
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI imekuwa mstari wa mbele kutambua mchango wa mwanamke na kuthamini jitihada zake katika kuleta mafanikio na kuhamasisha mabadiliko ya jamii kwa kuzingatia usawa wa Jinsia.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameyasema hayo Machi 7,2024 jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa ushirikiano na Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani machi 08.2024
Dkt. Gwajima ameitaka jamii kutumia makongamano kama fursa ya kuchochea wajibu wa wanawake kwenye maendeleo ya kiuchumi,Kijamii na kisiasa kitaifa na Kimataifa.
“Serikali kwa kushirikiana na Asasi mbalimbali imekuwa mstari wa mbele kuchochea harakati za kuimarisha, kutetea na kupigania maslahi ya wanawake kwa kuunganisha nguvu na sera kama familia moja.”amesema Dkt.Gwajima
Aidha amesema Serikali inaendelea kutoa wito kwa jamii nzima kutambua kuwa ujenzi wa Taifa lolote Duniani hauwezekani isipokuwa kwa ushirikiano kati ya mwanamke na mwanamume.
“Ni ukweli usiopingika kuwa wanawake ni msingi wa mabadiliko mbalimbali ikiwemo masuala ya kiuchumi. Hivyo, wasipopewa fursa si rahisi kabisa kwa taifa kuendelea.”amesema
Hata hivyo ameisihi jamii kwa ujumla kushirikiana ili kuendelee kuongeza kasi ya uelewa wa masuala ya jinsia kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya ndani ya jamii na hatimaye kuongeza kasi ya maendeleo.
Amesema wana mipango ya baadaye ya Taasisi hizi kushirikiana kikamilifu katika kutatua changamoto za wanawake na jamii kwa ujumla ambapo Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru itatumia mbinu shirikishi kuibua changamoto za wanawake na kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam watatafuta suluhu za changamoto kwa kutumia teknolojia.