Featured Kitaifa

MBUNGE MTATURU AMWAGA MITUNGI YA GESI JIMBONI

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amegawa mitungi ya gesi kwa viongozi wote wa jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambazo ni Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT), Umoja wa Vijana (UVCCM), na Jumuiya ya Wazazi.

Hatua hiyo ni muendelezo wa mkakati wake wa kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutumia Nishati safi ya kupikia.

Akigawa mitungi hiyo katibu wa Mbunge Ally Rehani amesema dhamira ya mbunge ni kuona wananchi wote wanatumia nishati mbadala ili kulinda mazingira na kuwa na afya njema kwa akina mama na wajasiriamali(mama na baba lishe).

Amewaomba viongozi kuendelea kupeleka elimu juu ya kutumia nishati mbadala na kutunza mazingira.

“Leo mhe Mtaturu amefikisha mitungi 300 aliyogawa kwa wananchi wa Singida Mashariki,”aliongeza. Katibu Ally Rehani.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi waliogawiwa mitungi hiyo, Mwenyekiti wa Wazazi Kata ya Ikungi Said Mkhandi amemshukuru mbunge kwa kuwawezesha kupata mitungi ya gesi kwani itakuwa chachu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

“Sisi wazazi jukumu letu mojawapo ni utunzaji wa mazingira,tunakushukuru sana mbunge wetu kwa kutuwezesha mitungi hii ya gesi,”.amesema.

About the author

mzalendoeditor