Kimataifa

TAKRIBANI WATU 15 WAMEUWAWA KATKA HUJUMA DHIDI YA KANISA NCHINI BURKINA FASO

Written by mzalendo

Takriban watu 15 waliokuwa kanisani wameuawa katika kijiji kimoja cha Burkina Faso wakati watu wenye silaha waliposhambulia eneo hilo la ibada siku ya Jumapili.

Wasimamizi wa kanisa wamesema vurugu hizo katika kijiji cha Essakane zilikuwa “shambulio la kigaidi” ambalo lilisababisha vifo vya watu 12 katika eneo la tukio, wakati wengine watatu walikufa baadaye walipokuwa wakitibiwa majeraha yao.

Abate Jean-Pierre Sawadogo, kasisi mkuu wa Jimbo Katoliki la Dori, ambapo shambulio hilo limejiri amesema watu kadhaa walijeruhiwa katika hujuma hiyo.

Hakuna kundi lilolodai kuhusika na hujuma hiyo, hata hivyo magaidi wakufurishaji hutekeleza mashambulizi kama hayo dhidi ya misikiti na makanisa nchini Burkina Faso.

Hujuma hiyo ya Jumapili ilitokea katika eneo ambalo makundi yenye silaha yamefanya mashambulizi kadhaa.

Takriban nusu ya Burkina Faso iko nje ya udhibiti wa serikali, kwani makundi yenye silaha yameharibu nchi hiyo kwa miaka mingi. Waasi na magaidi wameua maelfu ya watu na kupelekea  watu zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi, jambo linalotishia uthabiti wa taifa hilo ambalo lilikumbwa na mapinduzi mawili ya kijeshi mwaka 2022.

Kwa muongo mmoja sasa, Burkina Faso imekuwa ikikabiliana na machafuko yanayohusishwa na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na Daesh/ISIS.

Wanajeshi wa Ufaransa walikuwa nchini Burkina Faso kwa zaidi ya miaka kumi kwa kisingizio cha kuisaidia nchi hiyo kupambana na ugaidi. Hata hivyo, magaidi walipata nguvu zaidi wakati wa uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo.

Kutokana na hali hiyo, mwaka jana serikali ya kijeshi iliamuru wanajeshi wa Ufaransa kuondoka nchini mara moja. Russia sasa inaisaidia Burkina Faso katika mapambano yake dhidi ya ugaidi na kuna matumaini kuwa mashambulizi ya kigaidi yatapungua kwa kiasi kikubwa katika miezi ijayo.

About the author

mzalendo