Kimataifa

WAKULIMA MALAWI WATAKIWA KUINGIA KWENYE SOKO LA TUMBAKU NA SOYA

Written by mzalendo

Mamlaka husika nchini Malawi zimewataka wakulima wa ndani kuingia katika soko la tumbaku na soya nchini China ili kukuza akiba ya fedha za kigeni nchini humo na kuimarisha uchumi.

Mdhibiti wa Kilimo, Ugani na Huduma za Kiufundi Alfred Menifumbo ametoa wito huo huko Liongwe wakati wa Kongamano la Uwekezaji wa Kilimo.

Kongamano hilo ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya kilimo, utalii na uchimbaji madini iliyotangazwa na Rais Lazarus Chakwera wa nchi hiyo kwa lengo la kuonyesha fursa za uwekezaji katika sekta hizo. 

Mwenifumba amesema kuwa sekta ya tumbaku ya Malawi, inayoendeshwa kwa kiasi kikubwa na wakulima wadogo inaweza kufaidika pakubwa na soko la China na akawahimiza kujiunga na sekta hiyo ili kuboresha ubora wa tumbaku ya Malawi na kushindana na nchi nyingine.

Aidha ameashiria zao la soya linalolimwa Malawi na kusisitiza kuwa ipo haja kwa nchi hiyo kutumia fursa zilizopo kupata masoko huko China. 

Mdhibiti wa Kilimo, Ugani na Huduma za Kiufundi wa Malawi ameeleza kuwa nchi hiyo inaweza kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato yake ya fedha za kigeni kwa mara 20 hadi 30 ikiwa wakulima wa mazao ya biashara wenye mashamba makubwa wataingia kwenye sekta hiyo na kufikia soko la China, na kwamba wawekezaji waliopo wako tayari kuwasaidia wakulima wa ndani kupanua shughuli zao ili kukamata fursa za soko.

About the author

mzalendo