Featured Kimataifa

RAIS MWINYI AFUNGUZ MAFUNZO SADCOPAC ZANZIBAR

Written by mzalendo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kuufungua Mkutano wa Mafunzo wa Kuwajengea Uwezo Taasisi za Ukaguzi na Mabunge ya (SADCOPAC) unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Uguja Jijini Zanzibar leo 17-4-2024.(Picha na Ikulu)

Na.Mwandishi Wetu-Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa nchi wanachama za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa bara la Afrika, SADC, kuona haja za kuziimarisha taasisi zao zinazosimamia utawala bora zikiwemo Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mamlaka za kuzuwia Rushwa na Uhujumu Uchumi pamoja na Mabunge kuona haja ya kuzipatia wataalamu zaidi wa fani mbalimbali ili ziwe na upeo mkubwa zaidi wa kufanya uchunguzi kwa mujibu wa majukumu yao.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alizishauri taasisi hizo kuona umuhimu wa kufanya ziara za kimafunzo na kujengeana uwezo kwa kujifunza mbinu bora za kisasa kwenye utekelezaji wa majukumu yao, sambamba na kuendelea kutoa mafunzo zaidi.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wandege Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magaharibi, alipofungua Mkutano wa Mafunzo kwa Wajumbe na Wataalamu wa Kamati za SADCOPAC katika kupambana na rushwa, kuhamasisha uwazi na uwajibikaji kwa usimamizi wa mali zisizo rejesheka kwa kamati hizo. 

Alisema, Mkutano huo kwa Zanzibar ni fursa nzuri kwa Wataalamu wa ndani pamoja na Mabunge ya nchi wanachama wa SADC kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za kukabiliana na rushwa, kuongeza uwazi na uwajibikaji kutoka nchi nyengine za mataifa ya Afrika hasa ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Pia alieleza Mafunzo hayo kufanyika Zanzibar ni fursa ya kuitangaza Tanzania na kuwawezesha wageni kupata nafasi adhimu ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii, zikiwemo fukwe nzuri na Mji Mkongwe wa Zanzibar wenye hadhi ya urithi wa Dunia. 

Akizungumzia suala la mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, kuwepo kwa uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma na kuhimiza uwajibikaji kwenye utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika kukuza uchumi wa mataifa ya Afrika na kuimarisha huduma za jamii, Rais Dk. Mwinyi alisema ni mambo ya misingi na yenye mchango muhimu kwa kuchochea kasi ya maendeleo ya mataifa hayo.

Alisema, rasilimali zilizomo Afrika ni vyanzo muhimu vya kukuza uchumi wa mataifa yao, ikiwa vitasimamiwa vyema na kutumika kwa misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji. Alisistiza kuwa taasisi za utawala bora zikiwemo Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mamlaka za kuzuwia Rushwa na Uhujumu Uchumi na Mabunge kwa nchi wanachama wa SADC yana mchango mkubwa wa kuyafikia matarajio ya mataifa yao.

Alisema, Serikali zote mbili za SMZ na SMZ zimejitahidi kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuhimiza uwazi na uwajibikaji ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 pamoja na mipango mingine ya maendeleo. 

Akitaja hatua hizo Rais Dk. Mwinyi alieleza ni pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zake kwa mafunzo ili kuzipatia weledi, kuzipatia vifaa vya kufanyia kazi na kuzijengea miundombinu bora ili zifanye kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alisema, inaendelea kupambana na rushwa, kuhimiza uwajibikaji na uwazi kwa kuanzisha mifumo mbalimbali ya huduma zikiwemo za kifedha.

Aliongeza, kuanzisha utaratibu wa kusomwa kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hadharani kwa kujadiliwa kwa kina na uwazi kwenye Baraza la Wawakilishi. 

Alieleza, hatua hiyo imeimarisha Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka zimesaidia sana kufikia malengo ya nchi kwa kuimarisha utawala bora.

Akiizungumzia sheria ya Ukaguzi wa Mapato na Matumizi ya Umma nambari 7 ya mwaka 2023 ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alieleza imeleta mafanikio makubwa kwenye kujenga uwelewa kwa wananchi juu ya matumizi ya fedha za Umma.

Kuhusu mafanikio hayo Rais Dk. Mwinyi alieleza ni pamoja na kutumia mifumo, kuokoa fedha za Serikali kwa asilimia 86.3, kutekeleza miradi ya maendeleo kwa uwazi kwa asilimia 96, kuongezeka kwa uelewa wa usimamizi wa fedha za umma (mapato na matumizi) kwa asilimia 96, Matumizi ya mifumo kwenye shughuli za Serikali pia yameongezeka kutoka asilimia 48 na kufikia 92.4

Mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na kuimarika kwa utendaji huo Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali kupewa kazi ya kusimamia na kufuatilia matumizi ya miradi ya maendeleo kupitia USAID na ADB ambapo awali kazi hio ilifanywa na taasisi binafsi.   

Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisema, Zanzibar inajitahidi kutekeleza kwa ukamilifu makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi wanachama wa kamati za SADCOPAC.

“Siku siku zote tutajitahidi kuwa kinara katika utekelezaji ili malengo na mipango yetu iweze kufanikiwa kama sote tunavyotarajia” alibainisha Rais Dk. Mwinyi.Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi alizitaka kamati za Mabunge ya nchi wanachama wa SADC, kuendelea kudumisha ushirikiano na Tanzania hasa Zanzibar.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara zinazosimamia sheria na utawala bora Tanzania, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Zanzibar pamoja na Uongozi na Sekretarieti ya SADCOPAC.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR

BAADHI ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania wa Kamati mbalimbali za Bunge wakifuatila hutuba ya Ufunguzi wa Mkutano wa mafunzo ya kuwajengea uwezo pamoja na  ufanyajikazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge ya (SADCOPAC) wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akifungua na kuufungua mkutano huo unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar leo 17-4-2024.(Picha na Ikulu)

WASHIRIKI wa Mkutano wa Mafunzo wa kuwajengea uwezo pamoja na ufanyaji kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge ya (SADCOPAC) wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia na kuufungua mkutano huo, unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar leo 17-4-2024.(Picha na Ikulu)

BAADHI ya Makatibu Wakuu wa SMZ wakifuatilia hutuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Mafunzo wa kuwajengea Uwezo Taasisi za Ukaguzi na Mabunge ya (SADCOPAC) wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia na kuufungua mkutano huo unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar leo 17-4-2024.(Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kuufungua Mkutano wa Mafunzo wa Kuwajengea Uwezo Taasisi za Ukaguzi na Mabunge ya (SADCOPAC) unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Uguja Jijini Zanzibar leo 17-4-2024.(Picha na Ikulu)

About the author

mzalendo