Featured Kitaifa

TOENI ELIMU YA SARATANI KWA WANANCHI; DKT NDUNGULILE

Written by mzalendoeditor

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imetoa rai kwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kuongeza kasi ya utoaji elimu ya ugonjwa wa Saratani kwa jamii ili kuchukua tahadhari na kuwahi matibabu kwa wakati.

Rai hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Faustine Ndugulile leo Februari 23, 2024 akiiongoza Kamati hiyo kufanya ziara ya kuona hali ya utoaji huduma za Afya, maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma ikiwemo na miradi ya afya inayotekelezwa na Taasisi hiyo.

Dkt. Ndungulile amesema kuwa jamii ikiwa na elimu ya kutosha juu ya ugonjwa wa Saratani watapata muamoko wa kuwahi Hospitali na kupata matibabu sahihi kwa wakati.

“Hivyo kuna haja ya kutanua huduma za Saratani kuwa zinapatikana katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda ili kupunguza adha ya wananchi kusafiri mwendo mrefu na kutumia gharama kubwa kufata huduma hizo Dar es Salaam.

Audha ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuboresha miundombinu na kuwa wabunifu katika kuzalisha mionzi tiba itakayotumika nchi nzima na Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya afya na kuifanya Tanzania kitovu cha tiba utalii Afrika Mashariki .

“Uwekezaji huu mkubwa alofanya Dkt Samia unalenga kuinufaisha nchi katika kuongeza pato la taifa kwani tutapata fedha za kigeni kwa kwa kuwauzia nchi jirani mionzi inayozalishwa hapa Ocean Road “, ameeleza Dkt Mollel

About the author

mzalendoeditor