Ofisi ya rais ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema Waziri mkuu wa nchi hiyo Jean-Michel Sama Lukonde, alijiuzulu siku ya Jumanne na kusababisha kuvunjwa kwa serikali yake.
Lukonde aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Felix Tshisekedi siku nane baada ya kuthibitishwa kwa mamlaka yake kama naibu wa kitaifa ambapo kwasasa atajiunga na bunge kama mjumbe.
“Ombi lake la kujiuzulu limekubaliwa. Hata hivyo, rais ameiomba serikali (ya Lukonde) kuendelea kushughulikia masuala ya kitaifa hadi serikali mpya itakapoundwa,” ofisi ya rais ilisema katika taarifa nyingine baadaye Jumanne.
Taarifa hiyo hata hivyo haikueleza sababu za Lukonde kujiuzulu.
Lukonde aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, yenye utajiri wa madini, mnamo Februari 2021.