Maafisa wa magereza nchini Urusi wamesema kiongozi wa upinzani mwenye umri wa miaka 47 Alexey Navalny, ameaga dunia, licha ya taarifa rasmi haijaweza kuthibitishwa na vyanzo huru.
Vyombo vya habari vya Urusi vimewanukuu maafisa kadhaa wa Huduma za Magereza za Serikali Kuu wakisema Navalny, kiongozi machachari wa upinzani hasimu wa Rais Vladimir Putin, alifariki Ijumaa huko katikati mwa Urusi baada ya kuwa mgonjwa alipokuwa akitembea.
Wanasema kuwa madaktari waliitwa lakini hawakuweza kumuokoa baada ya kupoteza fahamu.
Maafisa wanasema uchunguzi umeanzishwa kufahamu chanzo kilchopelekea kifo cha kongozi huyo wa upinzani.
Navalny alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 19 jela kwa mashtaka ya msimamo mkali sana.
Alihamishwa kutoka jela ya zamani alikokuwepo katika mkoa wa Vladimir katikati ya Russia na kwenda katika jela yenye ulinzi mkali huko mjini Kharp, katika mkoa wa Yamalo-Nenets, kiasi cha kilomita 1,900 kaskazini mashariki mwa Moscow.