Na Mwandishi Wetu; Dodoma
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Mashirika ya Maendeleo wamekutana leo jijini Dodoma katika kikao cha wadau wa utatu ili kujadili na kupokea maoni kuhusu nchi kuridhia mikataba sita ya ILO.
Akifungua Februari 13, 2024 kikao hicho kilichohudhuriwa na wadau wa utatu kutoka Zanzibar, Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Said Mabie amesema mikataba hiyo iliyopendekezwa kwa maridhiano ni pamoja na Mkataba wa Hifadhi ya Jamii; Mkataba wa Mafao ya Wafanyakazi wanaopata Majanga yatokanayo na Kazi; Mkataba wa Sera ya Ajira Mahala pa Kazi; Mkataba wa Mfumo wa kuhamasisha Masuala ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi; Mkataba wa Wafanyakazi wa Majumbani na Mkataba wa Wafanyakazi wa Majumbani.
Naye, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya ametoa rai kwa washiriki wa kikao hicho kutumia fursa hiyo kuipitia mikataba yote na kutoa maoni yatakayoimarisha masuala ya kazi na ajira.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi wa Programu wa ILO, Edmund Moshy amesema shirika hilo lipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu ili kutimiza malengo wafanyakazi.