Kimataifa

SERIKALI INATHAMINI UZALENDO NA MCHANGO WA HAYATI LOWASSA – DKT. MPANGO

Written by mzalendo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.
Philip Mpango amewaongoza viongozi na wananchi katika kutoa heshima za
mwisho kwa Waziri Mkuu Mstaafu hayati Edward Ngoyai Lowassa katika
viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam.

Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais ametoa pole kwa
familia, ndugu, marafiki pamoja na watanzania wote kwa ujumla kufuatia
msiba huo mkubwa kwa Taifa.

Makamu wa Rais amesema serikali inathamini uzalendo na mchango mkubwa
aliyoutoa Hayati Edward Lowassa katika maendeleo ya nchi kwa kuwa
alijitolea kwa dhati kulitumikia Taifa pamoja na kutumia vema karama
alizojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia Watanzania katika nyadhifa
mbalimbali alizowahi kushika.

Amesema ni muhimu kila mmoja mtanzania
kujikumbusha wajibu aliyonao kwa taifa na kuyaishi kwa vitendo mambo yote
mazuri yanayotokana na maisha ya hayati Lowassa.

Amesema ni vema Watanzania kumuenzi hayati Lowassa kwa kuendelea
kuchapa kazi ili kuboresha maisha na hivyo kuchangia katika ujenzi wa Taifa
kwa kuwa alikuwa mchapa kazi hodari katika utumishi wa umma na katika
shughuli zake binafsi ikiwemo ufugaji.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa watanzania wote na hususan vijana
kumuenzi hayati Lowassa kwa kutumia fursa mbalimbali kujipatia elimu kwa
manufaa ya Taifa kwa kuwa alikua kinara katika elimu na kusimamia kwa
uhodari utekelezaji wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ya elimu
hususan ujenzi wa shule za Sekondari kila Kata.

Makamu wa Rais amesema Hayati Edward Lowassa alikuwa mwanamazingira
hodari ambapo katika wadhifa wake wa Waziri wa Nchi – Ofisi ya Makamu wa
Rais na alipokuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
alihimiza sana uhifadhi na Utunzaji wa mazingira.

Aliongoza kampeni nyingi za upandaji miti na usafi wa mazingira. Amesema mchango wake huo uwakumbushe watanzania wote wajibu wa msingi wa kulinda na kutunza
mazingira na hususan vyanzo vya maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko
ya tabianchi ambazo zinaendelea kuleta madhara mengi katika Taifa na dunia
kwa ujumla.

Vilevile Makamu wa Rais amesema Hayati Edward Lowassa alikuwa na bidii
katika kumwabudu Mwenyezi Mungu akiwa msharika mzuri, akisali mara
nyingi katika kanisa la KKKT Azania Front. Amesema mfano huo ikumbushe
kuwa kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa na msingi wa mafanikio katika
familia na katika utumishi wa umma.

Makamu wa Rais amewasihi watanzania kutumia msiba huo kudumisha na
kuimarisha upendo, amani na mshikamano wa Taifa.

 

About the author

mzalendo