Featured Kitaifa

TANROADS FANYENI KAZI KWA USHIRIKIANO

Written by mzalendo

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta, akizungumza na Wajumbe wa Baraza wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Baraza la wafanyakazi wa TANROADS, leo tarehe 13 Januari 2024 Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la  Wafanyakazi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Mhandisi Mohamed Besta wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Baraza hilo leo tarehe 13 katika ukumbi wa St. Gaspar Jjini Dodoma.

……..

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi amewataka watumishi wa wakala huo kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano baina yao ili kuleta tija na ufanisi kwa Wakala huo.

Mhandisi Besta amezungumza hayo leo Februari 13, 2024 wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Baraza la wafanyakazi lililofanyika jijini Dodoma.

“Nawaomba tuendelee kufanya kazi kwa pamoja kama ndugu kwa sababu sisi ni familia moja na kazini ni sehemu ambayo inatakiwa iwe na upendo ili kuweza kusaidiana katika kutatua changamoto za kazi na hata za kijamii”, amesema Mhandisi Besta.

Vilevile amewapongeza Watumishi wa Wakala huo kwa muda mchache aliokaa nao amepata ushirikiano wa kutosha kutoka katika Timu ya TANROADS ambayo inafanya kazi kwa kutegemea Weledi, Utu na Undugu.

Aidha, ameushukuru Uongozi wa Wizara ya Ujenzi ambao ni waongoza sera kwa kuendelea kufanya nao kazi kwa ukaribu na kwa ushirikiano ili kuhakikisha malengo ambayo yamewekwa yanafikiwa na yanatekelezeka.

Ameongeza kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali cha kuweza kuajiri zaidi ya Watumishi 2400 ambao walikuwa wakifanya kazi kwa mkataba katika taasisi hiyo.

“Kipindi naingia Taasisi yetu ilikuwa na wafanyakazi Takribani 755 ambao walikuwa wameajiriwa ajira za kudumu na wengine zaidi ya 2000 walikuwa wameajiriwa ajira za Mkataba, Uongozi umefanya juhudi na sasa wafanyakazi wote waliokuwa kwenye ajira za mikataba,wamepata ajira za kudumu”, aliongezea Besta.

Pia ameeleza kuwa  Wakala unaendelea kuboresha maslahi kwa jinsi hali itakavyokuwa nzuri wataweza kuendelea kutoa ajira kwa kuzingatia uchumi wa Nchi.

Mkutano wa 19 wa Baraza la wafanyakazi, unafanyika Dodoma kwa Siku 2 na kushirikisha zaidi ya wajumbe 100 kutoka Mikoa yote ya Tanzania.

About the author

mzalendo