Featured Kitaifa

BMH YAPOKEA GARI ZA KUBEBEA WAGONJWA

Written by mzalendo
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma imepokea magari mawili (2) ya kubebea wagonjwa kutoka Serikalini yatakayosaidia utoaji wa huduma nzuri zaidi kwa watanzania.
Akiongea leo baada ya hafla  ya kupokea magari hayo, Mbunge wa Dodoma mjini, Anthony Mavunde, amesema magari hayo yataondoa changamoto ya mgonjwa anapopata rufaa.
“Naishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa  kuboresha huduma ya Afya,” amesema Mbunge wa Dodoma mjini.
Ameongeza msaada huo wa magari ya wagonjwa ni muhimu sana kwa BMH kwani Hospitali imekuwa kimbilio sio tu kwa wakazi wa Dodoma bali kwa watanzania kwa ujumla.
Mkuu wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema msaada huu wa magari ya wagonjwa unaonyesha dhamira ya dhati ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha huduma ya Afya.
“Tutasimamia magari haya yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kubeba wagonjwa,” amesema Mkuu wa Mkoa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Dkt Alphonce Chandika, ametoa shukrani kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuipatia Hospitali hii ya Kanda ya Rufaa magari hayo mawili ya wagonjwa.
” Ni furaha kwa BMH kupata msaada huu wa magari ya wagonjwa. Tunamshukuru sana Mhe Rais kwa msaada huu,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharula, Dkt George Dilunga, ameeleza kuwa magari haya yamefungwa vifaa maalumu ambavyo vinamuwezesha mtoa huduma kutoa huduma wakati wakiwa kwenye gari.

About the author

mzalendo