Featured Kitaifa

MBUNGE MTATURU:RAIS SAMIA APEWE MAUA YAKE,ANASIMAMIA VYEMA FALSAFA YA 4R.

Written by mzalendo

 

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu,akichangia Miswada ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023,Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023 bungeni jijini Dodoma.

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwak uwa msikivu na kusimamia falsafa yake ya 4R ya kuwa na maridhiano,mageuzi,ustahimilivu na kujenga upya Taifa.

Akichangia Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023,Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023,Januari 30,2024 Bungeni Jijini Dodoma Mtaturu amesema:

“Pongezi kwa Rais wetu,kwenye hili yeye ndio kinara,bila ya kupepesa macho kama asingekuwa Rais Msikivu na anayependa kuona mabadiliko Sheria isingekuja hapa, tungeishia kupiga kelele, tungeishia kuwa na mbwembwe na kila aina ya sarakasi,lakini kama yeye asingekubali Sheria isingekuja,kwa hiyo sisi watanzania lazima tuone aina ya Rais tuliyenaye.”

“Kupitia mfumo wake wa 4R anaonyesha wazi kiongozi anatakiwa kuwa wa namna gani,hata kama jambo linakusumbua ,linakuuma lazima ukubali uweze kuvumilia,usikilize hoja za watu wengine,kwa hiyo kwenye hili Mh Rais amefanya jambo kubwa la kuiponya Nchi ,anaenda kuipeleka Nchi kwenye maridhiano ya vitendo,katika hili tumpe Rais maua yake,”amesema.

Ameeleza kuwa kazi anayoifanya Rais Samia ni kuipeleka Tanzania kwenye maridhiano ya kweli ambayo yanaweza kuletwa na Sheria ili hata kama yeye akiondoka baada ya uongozi wake anaweza kuacha Sheria ya Uchaguzi ambayo inaendeshwa katika sura ya maridhiano.

Mtaturu ameweka bayana mambo ambayo Rais Samia ameyafanya ikiwemo kuruhusu Baraza la Vyama vya Siasa vikutane waweze kujadili hali iliyoongeza wigo mpana kwa maeneo ambayo yalikuwa hayapo kwenye Sheria.

Amesema hilo amelifanya ili apate mawazo mbalimbali ya watanzania na wadau mbalimbali ambao walishirikishwa wakiwemo asasi za kiraia,viongozi wa dini na makundi mbalimbali.

“Mh Rais alitaka watanzania wote washiriki katika kujenga Nchi yao,kama walivyosema wabunge wengine kwamba siasa ikiendeshwa vizuri hata maendeleo yatapatikana,kwa hiyo mimi nataka kusema kupitia mwongozo wa Mh Rais na kukubali haya yote tunaiona tanzania tunayoitamani inakuja ya watu wote kukaa kwa pamoja,

“Mh Rais,ameweza hata kwenda kushiriki kwenye mikutano ya vyama vya upinzani na akazungumza nao na wakafurahia kumuona kama ni sehemu yao, hili ni jambo kubwa ambalo amelionyesha,”.amesema.

Amesema katika eneo hilo pia kuliundwa kikosi kazi ambacho kilichambua maoni kutoka Baraza la Vyama vya Siasa na wlaikusanywa wasomi ,viongozi wa dini ,vyama vya siasa,makundi mbalimbali yalipata nafasi ya kutoa maoni na ndio yalizaa mapendekezo ambayo yanaongelewa kwenye Miswada ya Sheria hizo.

“Nimeambiwa hapa asilimia zaidi ya 80 ya maoni yaliyokuwa yametajwa yameingizwa kwenye sheria ambayo kiukweli ndio mawazo ya wadau mbalimbali wa vyama vya siasa,hakika bado tunaendelea kumpongeza Mh Rais na serikali yote,kuna baadhi ya mambo unaweza kuwa unafanya kama kiongozi lakini baadae unageuka,

“Ni kama wewe una mgeni nyumbani kwako unatenga chakula unaenda kuleta maji ya kunawa,wakati unaenda kuchukua maji unarudi unakuta mgeni wako yuko juu ya meza anakanyaga chakula ,sasa wakati sisi tunahangaika kuletwa miswada hii bungeni tumeona wengine wanaanza kufanya sarakasi barabarani hii ni sawa sawa na mgeni huyo anayekanyaga chakula kwa viatu,utamuangalia kwa sura gani,

Mtaturu amesema pamoja na sarakasi za huyo mgeni lakini Rais Samia amekubali Miswada hiyo ijadiliwe ili kuweza kutengeneza Sheria ya Uchaguzi iliyo nzuri.

“Kwa hiyo nataka niseme, uvumilivu wa Mh Rais ni wa kiwango cha juu kabisa ni Rais ambaye kwa hakika dunia yote inamtazama,ameruhusu maandamano ,wamepeleka hisia zao ,wamepeleka barua huko walikopeleka ingawa wamesema ilikuwa haijasainiwa lakini yote bado waliendelea kusikilizwa na leo tupo na Miswada hii ya Sheria ambayo itaenda kutupeleka kwingine,”ameongeza.

Mtaturu ameipongeza pia Kamati ya Kudumu ya bunge ya Utawala,Katiba na Sheria pamoja na serikali kwa wasilisho zuri ambalo limejenga uelewa na kuchambua baadhi ya mambo yaliyokuwa yamejificha ndani ya miswada hiyo.

About the author

mzalendo