Featured Kitaifa

CFAO MOBILITY YAFANYA MAONESHO YA MAGARI MAPYA KUCHOCHEA MAENDELEO YA TEKNOLOJIA

Written by mzalendoeditor
CFAO Mobility, kampuni kinara katika sekta ya usafirishaji barani Afrika imeandaa Maonesho ya Magari yaliyofanyika Jumamosi, Januari 20, 2024 katika uwanja wa Greens Ground jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo ya kipekee yaliondaliwa kwa ustadi mkubwa yamelenga kuboresha sekta ya magari na usafirishaji nchini Tanzania kwa kutambulisha teknolojia za kisasa kwa wadau na washiriki wa maonesho hayo.

 
Maonesho hayo ya kipekee yamekwenda zaidi ya kuonesha magari na badala yake yamekuwa jukwaa la kuelimisha washiriki undani wa teknolojia za kisasa zinazotumika katika chapa maarufu kama Mercedes-Benz, Volkswagen, Fuso, na Suzuki. Kupitia Maonesho hayo, pia, washiriki walipata nafasi ya kujionea matoleo mapya kabisa ya magari hayo na kufanya majaribio ya kuyaendesha kwa lengo la kujionea utofauti. CFAO Mobility ni kampuni inayouza magari na vipuri vya magari mapya kabisa ya chapa za Mercedes-Benz, Volkswagen, Fuso na Suzuki; magari yanauzwa na CFAO Mobility hutengenezwa kuakisi mahitaji ya kipekee na mazingira ya Tanzania.
Katika maonesho hayo, wataalamu wabobevu wa chapa husika za magari kutoka CFAO Mobility walitoa elimu ya kina ya matoleo mbalimbali kwa washiriki. Washiriki pia walifurahia huduma za ukaguzi wa magari yao na kununua vifaa halisi kwa bei ya punguzo kutoka WinPart Tanzania ambalo ni duka la vipuri halisi lililo chini ya CFAO Mobility.
Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa CFAO Mobility Tanzania, Tharaia Ahmed alieleza lengo kuu la maonesho hayo yaliyopewa jina la ‘The Motor Show’ wakati wa hotuba yake, akisisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika kuinua sekta ya magari na usafirishaji nchini Tanzania kwa kuonyesha teknolojia za kisasa.
“Shukrani zetu za dhati ziwaendee wahudhuriaji wote kwa kufanikisha maonesho haya. Tukio hili tumelitumia kama jukwaa la kuungana na wateja wetu, kuonesha matoleo mapya ya magari yetu, na kukusanya maoni kwa lengo la maboresho. Kama kampuni kinara barani Afrika, lazima tuendelee kuhakikisha watu wetu wanafahamu na kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya magari na usafirishaji yanayotokea kwa kasi kubwa duniani. Matokeo chanya yanayptokana na tukio hili yanatutia moyo kuendelea kutoa huduma za kipekee nchini Tanzania,” alisema Bi Ahmed.
 
 
Washiriki wa maonesho hayo walipata maarifa mengi kuhusu uvumbuzi na teknolojia mpya za magari. Mshiriki ambaye alijitambulisha kama mpenziwa magari chapa ya Volkswagen alisifu tukio hilo, akisema, “Elimu kuhusu chapa mbalimbali za magari imenifungua sana kufahamu mambo mengi kuhusu magari husika. Kwa upande wa huduma, nimefurahia sana huduma ya bure ya ukaguzi wa matairi ambayo pia imethibitisha kwamba CFAO wanajali sana wateja wake. Zaidi ya matarajio yangu, nimepata pia fursa ya kuendesha kwa majaribio matoleo ya hivi karibuni ya Vokswagen na hii imenipa furaha sana!” alisema.
 
 
Tukio la Maonyesho ya Magari ni mwendelezo wa juhudi za CFAO Mobility kuwaleta Watanzania karibu na magari na huduma za kisasa, salama na endelevu. Maonesho haya yameacha alama kwenye sekta ya magari na usafirishaji nchini Tanzania kwa kutambulisha teknolojia za kisasa za magari.

About the author

mzalendoeditor