Featured Kitaifa

VIJANA SONGWE WATAKIWA KUTOJIHUSISHA NA VITENDO VYA KIHALIFU

Written by mzalendo

Na Issa Mwadangala

Vijana wametakiwa kutojihusisha na vitendo vya kihalifu ambavyo vinapelekea kurudisha nyuma maendeleo katika jamii.Kauli hiyo ilitolewa Januari 20, 2024 na Polisi kata wa kata ya Ruanda Mkoani Songwe Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Happy Lumbe alipofanya mazungumzo na kutoa elimu kwa wananchi wa kata hiyo.

Amesema baadhi ya vijana ambao ni tegemeo kubwa kwenye jamii katika shughuli za kimaendeleo wanafanya vitendo vya kihalifu ikiwemo kuiba mizigo ya watu iliyopakiwa kwenye magari makubwa yanayoingia ndani ya nchi na yanayotoka nje ya nchi ambayo yanapita kwenye barabra ya Mbeya/Tunduma ambayo imepita kwenye kata hiyo.

“Ni jambo la ajabu kwa kijana ambae ana nguvu za kutosha kushusha mzigo kwenye gari la mtu huku akijua kwamba mzigo huo sio mali yake, lakini nataka mtambue kuwa kufanya hivyo ni kosa na sheria itachukua mkondo wake kwa atakaebainika” alisema  mkaguzi huyo.

Aidha aliwasisitiza vijana hao kutumia nguvu zao katika kufanya kazi ili kupata kipato cha halali  badala ya kufanya matendo yanayoenda kinyume na sheria ambayo yanaweza kuwaletea athari ikiwa pamoja na kufikishwa mahakamani.

Nao wananchi wa Kata hiyo wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi zake za kuwatumia Polisi kata kutoa elimu katika majukwaa mbalimbali nchini.

About the author

mzalendo