Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

CHUO Cha Mipango Ya Maendeleo Vijijini (IRDP) inatarajia kuanza kutuo mafunzo ya kozi mbili mpya zinazohusiana na biashara ili kusaidia kuzalisha wataalamu wenye weledi wa juu katika sekta ya mipango ya maendeleo nchini.

Kozi hizo ambazo zitaanza kutolewa katika mwaka wa masomo wa 2024/25 katika ngazi za cheti na stashahada ni pamoja na Uhasibu na Usimamizi wa Fedha, na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), na zitafundishwa kwa namna maalum itakayoendana na masuala ya mipango ya maendeleo.

Kuanzishwa kwa kozi hizo muhimu ambazo tayari zimepitishwa na Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kunatokana na utafiti wa kina uliyofanywa na Chuo hicho, ambapo ulibaini kuwa wataalam wengi wa mipango ya maendeleo nchini Tanzania hawana maarifa na ujuzi wa kutosha juu mambo ya ICT, pamoja na Uhasibu na Usimamizi wa Fedha.

Naibu Mkuu wa IRDP, Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa Provident Dimoso ameieleza ‘Semaswahili’ wakati wa mahojiano maalum kuwa lengo ni la kuanza kwa kozi hizo ni kuhakikisha wataalam watakaozalishwa wanatumia ipasavyo na kitaaluma matumizi ya TEHAMA na Uhasibu na Usimamizi wa Fedha ili kuboresha utendaji wa sekta ya mipango ya maendeleo nchini.

“Kuanza kutolewa kwa programu hizi kunalenga haja ya kukidhi mahitaji ya sasa ya soko kwani waajiri wengi wamekuwa wakiibua wasiwasi wa kukosa wataalam wa maswala ya mipango ya maendeleo wenye ujuzi juu ya maeneo hayo mawili muhimu, ” Profesa Dimoso alieleza.

Ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya kimsingi kabla ya utoaji wa programu hizo, alieleza kuwa chuo hicho kinachomilikiwa na serikali tayari kimeajiri wakufunzi wa hali ya juu ili kuwafundisha wanafunzi watarajiwa ambao watajiunga katika kozi hizo.

“Mbali na kuajiri wakufunzi wapya, pia tumefadhili baadhi ya walimu wetu kupata ujuzi unaohitajika kutoka nje ya nchi ili kuhakikisha tunasimama upande wa kitaaluma zaidi kuzalisha wataalam bora ambao watakidhi mahitaji ya sasa katika upande wa mipango ya maendeleo ya nchi,” aliongeza.

Si hivyo tu, lakini Profesa Dimoso alisema tayari Chuo kimeanzisha maktaba ya kisasa ya kompyuta iliyounganishwa na mfumo wa kisasa wa intaneti kwa ajili ya kuwezesha mafunzo mazuri kwa wanafunzi, hasa wale watakao soma kozi za TEHAMA.

Amesema, maktaba hiyo imewekwa jumla ya kompyuta za kisasa takribani, na programu tofauti zinazohusiana na masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

“Pia, tumeingia mkataba na Mtandao wa Utafiti Tanzania (TERNET) kwa lengo la kutupatia huduma za mtandao wa haraka na wa uhakika katika maktaba hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa nzuri ya kujifunza kitaalamu zaidi,” alibainisha.

Kupitia mkataba huo, amesema Chuo kitakuwa kinapata angalau Megabiti 1000 kwa sekunde (MBPs), pamoja na huduma zingine zinazopatikana za bando za intaneti kutoka makampuni mengine makubwa, ikiwa ni pamoja na TTCL, ZANTEL na TIGO.

Profesa Dimoso alisema Chuo hicho kwa sasa kinafanya kazi ya kuboresha kitabu cha muongozo wa udahili wa wanafunzi kwa lengo la kuweka vigezo na sifa ambazo waombaji wanapaswa kuwa nazo ili waweze kujiunga na kozi hizo mpya.

Pamoja na hayo, IRDP pia imeanzisha programu maalum ya kutoa kozi fupi tofauti tofauti zenye lengo la kuwajengea uwezo wafanyakazi wa serikali kuu, tawala za mikoa na serikali za mitaa, taasisi za umma, pamoja na wale wanatoka kwenye mashirika binafsi.

Previous articleMAJALIWA ASHIRIKI MKUTANO WA TATU WA KUSINI WA KUNDI LA 77 NA CHINA
Next articleVIJANA SONGWE WATAKIWA KUTOJIHUSISHA NA VITENDO VYA KIHALIFU

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here