OR-TAMISEMI
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeipongeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kusimamia kikamilifu miradi ya elimu inayotekelezwa katika halmashauri mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Denis Londo kwenye ziara ya kamati ya kukagua miradi ya elimu na miundombinu inayotekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Wilaya ya Iringa na Mufindi mkoani Iringa.
Mhe.Londo amesema Kamati imeridhishwa na ujenzi wa miundombinu ya elimu na kupongeza Ofisi hiyo kwa kazi kubwa ya kutekeleza miradi hiyo.
“Rai yangu kwa wataalamu wetu nchini kote ni kuhakikisha wanatumia taaluma zao katika kushauri kwenye kila mradi ambao unatekelezwa na serikali. Watendaji wetu ndio mnapaswa kuwa wa kwanza kuyaona mapungufu na kuyarekebisha na siyo kusubiri ije kamati ya bunge ama viongozi wa kitaifa ndio waje kuona mapungufu,”amesema.
Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe.Deogratius Ndejembi ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea na kukagua miradi hiyo huku akiahidi kuchukua maelekezo yote yanayotolewa ili kuboresha zaidi katika miradi mingine inayotekelezwa na serikali kupitia TAMISEMI.
Kamati hiyo inaendelea na ukagua wa miradi iliyopo chini ya TAMISEMI katika Mkoa wa Iringa na Mbeya.