Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watuhumiwa sita (06) wanaodaiwa kushiriki katika tukio la uvunjaji na unyang’anyi lililotokea katika maeneo ya Dole na Mwanyanya Wilaya ya Magharibi A” mkoa wa Mjini Magharibi.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, 02 Januari 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi ACP. Richard Thadei Mchomvu, amesema mnamo tarehe 30 Disemba 2023 majira ya saa 8:00 usiku huko Dole na Mwanyanya, wahalifu hao walivunja nyumba sita za wananchi na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo simu 18, Kompyuta, Tv pamoja na fedha taslimu Tshs. 85,000.
“Watuhumiwa hao ambao wanakadiriwa idadi yao kuwa 10 waliiba vitu pamoja na kuwajeruhi wananchi wa maeneo hayo, ambapo jumla ya wanachi 15 walijeruhiwa na kati yao wanne walilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja kwa ajili ya kupatiwa matibabu” alisema kamanda Mchomvu.
Ameeleza kwamba jitihada za Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi zimesaidia kuwakamata watuhumiwa hao na msako mkali wa kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wengine wa tukio hilo unaendelea.
“Tunaenda vizuri, tunashirikiana na mikoa mingine ili kuweza kuwakamata watuhumiwa hao ambao umri wao ni kati ya miaka 13 hadi 30” amelisema Kamanda Mchomvu
Aidha, amekemea baadhi ya wananchi kutumia mitandao ya kijamii kinyume na utaratibu jambo ambalo linapelekea taharuki kwa wananchi. Akifafanua kuhusiana na tukio hilo amesema sio jambo la kimaadili kutumia mitandao ya kijamii kuonesha vitu ambavyo vipo kinyume na maadili.
Kuhusu suala la usalama alisema “Ulinzi uliimarishwa na sikukuu za Christismas, ufunguzi wa uwanja wa New Amaan Complex na Mwaka mpya zimepita salama. Hivyo niwatake wananchi kuendelea kutii sheria katika kipindi hiki tunacheolekea maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ambayo kilele chake yatakuwa tarehe 12 Januari 2024” amesema kamanda Mchomvu
Mafanikio ya utii wa sheria kwa wananchi ni matunda ya elimu mbalimbali za ushirikishwaji wa jamii zinazotolewa kwa wananchi wa maeneo husika, hivyo amesisitiza wananchi kuwa sehemu ya vikundi vya Ulinzi Shirikishi ili kuzuia uhalifu.