Featured Kitaifa

WAZIRI JAFO AONGOZA ZOEZI LA UPANDAJI MITI DODOMA

Written by mzalendo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipanda mti katika zoezi lililoandaliwa na Taasisi ya Habari Conservation Organisation na Benki ya NMB katika eneo la Mnadani Msalato jijini Dodoma leo Desemba 23, 2023.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akimwagilia mti alioupanda katika zoezi lililoandaliwa na Taasisi ya Habari Conservation Organisation na Benki ya NMB katika eneo la Mnadani Msalato jijini Dodoma leo Desemba 23, 2023. Anayeshuhudia kulia ni na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Khamis Mkanachi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwanawisha watendaji wa Benki ya NMB mara baada ya kupanda mti wakati wa zoezi lililoandaliwa na Taasisi ya Habari Conservation Organisation na benki hiyo katika eneo la Mnadani Msalato jijini Dodoma leo Desemba 23, 2023. Kushoto ni Mwenyekiti wa Habari Conservation Organisation Bw. Bernad James.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipanda mti na wadau wa mazingira wakati wa zoezi la upandaji wa miti lililoandaliwa na Taasisi ya Habari Conservation Organisation na Benki ya NMB katika eneo la Mnadani Msalato jijini Dodoma leo Desemba 23, 2023.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na wananchi mara baada ya kuongoza zoezi la upandaji wa miti lililoandaliwa na Taasisi ya Habari Conservation Organisation na Benki ya NMB katika eneo la Mnadani Msalato jijini Dodoma leo Desemba 23, 2023.

……………

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema ajenda ya upandaji miti inawahusu watu wote hivyo ni jukumu la kila mmoja kushiriki zoezi hilo.
Ametoa kauli hiyo wakati wa akizungumza na wananchi mara baada ya kuongoza zoezi la upandaji miti lililoandaliwa na Taasisi ya Habari Conservation Organisation kwa hisani ya Benki ya NMB katika eneo la Mnadani Msalato jijini Dodoma leo Desemba 23, 2023.
Dkt. Jafo amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yameleta athari kubwa katika nchi yetu hivyo ajenda ya utunzaji wa mazingira haihitaji kubembelezana hivyo kila mwananchi anapaswa kuiona ni ya kwake.

Amesema kuwa viongozi wakuu wa nchi wameelekeza zoezi la upandaji wa miti lifanyike nchi nzima na kwamba tunahitaji kupanda miti takriban milioni 276 kwa mwaka kwa halmashauri zote.

”Kama mnavyojua mabadiliko ya tabianchi yamekuwa ni changamoto kubwa sana duniani na hivi karibuni tulikuwa kwenye Mkutano wa COP28 unaona jinsi gani kila nchi inakuja pale inalalamika kuhusu mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame kutokana na ukosefu wa mvua,” amesema.

Waziri Jafo ametoa wito kwa wananchi kuitunza miti inayopandwa ili iweze kustawi na hivyo kufikia malengo ya Serikali ya kuhakikisha inakabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri uchumi.

Halikadhalika, Waziri Jafo amewapongeza wadau wa mazingira wakiwemo Taasisi ya Habari Conservation Organisation na Benki ya NMB ambao wamekuwa wakiunga mkono Serikali katika hifadhi ya mazingira.

Amewapongeza pia viongozi na wananchi kwa jitihada zao za kuibadilisha Dodoma kuwa ya kijani ambapo imewekewa lengo la kupanda miti milioni 40 kwa kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo, Waziri Jafo ameelekeza viongozi wa Jiji la Dodoma wanaosimamia mnada huo kuhakikisha eneo hilo linakuwa safi kwa kuondoa taka zinazorundikwa na kuzitupa kunakostahili.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Khamis Mkanachi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, amesema zoezi la upandaji miti litakuwa endelevu ili kuleta ufanisi.

Amesema ili zoezi hilo liwe endelevu viongozi wa ngazi za chini kuanzia mitaa na vijiji wanapaswa kuwasimamia wananchi wao kila kaya kupanda miti na kuitunza kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.

Ameshukuru taasisi mbalimbali kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za utunzaji wa mazingira kupitia zoezi la upandaji miti ambao wamekuwa wakitoa miche kwa ajili ya kupandwa.

Pia, kutokana na maelekezo ya Waziri Jafo, Mkuu wa Wilaya amesema amechukua hatua kwa kumuelekeza Afisa Mazingira wa Jiji la Mtendaji wa kata kushughulikia jambo hilo.

Nae Mwenyekiti wa Habari Conservation Organisation Bw. Bernad James amesema jumla ya miti 1,100 imepandwa katika eneo hilo la mnadani ikiwa ni katika kuunga mkono Serikali kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kila mwaka.

Amesema kuwa kwa miaka takriban mitatu iliyopita taasisi hiyo imefanikiwa kupanda miti milioni moja na elfu tatu ambapo ameiomba jamii iitunze miti hiyo hadi ikue na hivyo kufikia matarajio.

Bw. James ameongeza kuwa suala la upandaji miti liwe ni tabia kwani miti mingi inakatwa nchini Tanzania na hali hiyo inaweza kusababisha kugeuka kuwa jangwa.

About the author

mzalendo