Featured Kitaifa

TUSIWAFICHE WATOTO WENYE USONJI- DKT. MOLLEL

Written by mzalendoeditor

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa wananchi kutowaficha watoto wenye changamoto ya Usonji (autism) kwani wakipata malezi na mafunzo mazuri watasaidia kuleta matokeo chanya katika jamii.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Desemba 3, 2023 wakati akifungua Mkutano wa kimataifa wa Usonji (autism) uliofanyika katika kituo cha kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amesema, katika kusaidia kupambana dhidi ya changamoto hiyo, Rais Samia alipoingia madarakani aliongeza bajeti ya Wizara ya Afya mpaka kufikia Tirioni 6.7 iliyosaidia kununua MRI kwenye hospitali za kanda na CT-SCAN katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa zitazosaidia katika kugundua magonjwa mbalimbali ikiwemo autism.

Ameendelea kusisitiza kuwa, kupitia mpango wa Dkt. Samia Health Specialisation Programu tayari Dkt. Samia ametoa Bilioni 9 kwaajili ya kupeleka Wataalamu wa afya wasiopungua 300 nje ya nchi ili kupata ujuzi wa fani za kibingwa na ubingwa bobezi na kusisitiza mpango huu ni endelevu.

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, tatizo la usonji (autism) linaendelea kuongezeka nchini na Duniani kwa ujumla, huku akisema mwaka 2021 katika kila watoto 44 mtoto mmoja alikuwa na changamoto ya autism lakini kwa mwaka 2023 katika kila watoto 36 mtoto mmoja ana autism.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, watoto wenye changamoto ya Usonji (autism) wanatakiwa uangalizi wa karibu na kukuza vipaji ili vyao vya uvumbuzi, ili kuleta tija katika jamii.

“Kuna wanasayansi wakubwa Duniani ambao wamegundua mambo mbalimbali na binadamu wakayafurahia, baadhi yao walikuwa watoto wenye changamoto kama hii ya Usonji (autism).” Amesema Dkt. Mollel.

About the author

mzalendoeditor