Featured Kitaifa

REA YAWASHA MRADI WA BILIONI 25 WA KUPOZA NA KUSAMBAZA UMEME (IFAKARA SUB STATION)

Written by mzalendoeditor

*Na Mwandishi Wetu, Ifakara-Morogoro*

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) imewasha Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara ambacho kimegharimu shilling bilioni 25.

Akiwasha kituo hicho ambacho kimelenga kuongeza uwekezaji na uanzishaji wa viwanda kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero , Mh Dunstan Kyobya ameshauri kituo hicho kiitwe Samia Ifakara Substation.

Ameipongeza REA na EU kwa kuhakikisha kituo kimekamilika na kuwashwa kwani kinaenda kumaliza matatizo ya umeme katika wilaya ya Kilombero, Malinyi na Ulanga ambayo ni maeneo ya kimkakati ya kilimo na viwanda.

“Tunategemea kuongeza uwekezaji kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na vile vya kuchakata madini” amesema Mh Kyobya.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira na vyanzo vya maji ili kujihakikishia umeme wa uhakika katika mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kihansi na Kidatu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwashwa kwa kituo hicho kunaongeza upatikanaji wa umeme na hivyo kuwawezesha wananchi kukuza na kuboresha hali zao za kiuchumi kwa kufungua biashara mbalimbali kwa uwepo wa umeme wa uhakika katika maeneo hayo.

“Wananchi watumie upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kujiongezea kipato kwa kuwekeza na kuanzisha viwanda vya mazao ya kilimo na madini ambayo yanapatikana kwa wingi Kilombero, Ifakara, Ulanga na Malinyi,” amesema Mhandisi Olotu.

Naye Mbunge wa Kilombero, Aboubakar Asenga amewataka wananchi wa Jimbo hilo kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa umeme mkubwa kwa kuzalisha kwa wingi na kuanzisha viwanda vikubwa.

“Tunaishukuru serikali kwa kutimiza ahadi yake, ni wajibu wetu wananchi kutumia fursa hii ya upatikanaji wa umeme mkubwa kwa kuwa na viwanda vya kukausha na kukoboa mpunga, uzalishaji wa matofali kwa kisasa na uongezaji thamani wa madini ili kujiongezea kipato, ” amesema Mh Asenga.

Meneja wa Mradi huo kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena amesema ujenzi wa kituo hicho ulianza 2020 ambapo kinazalisha kV 220 za umeme baada ya wananchi wa maeneo hayo kuwa wanapata umeme mdogo wa kV 33 uliokuwa unasababisha kukatika mara kwa mara.

Na baada ya kuwashwa kwa kituo hicho, kutawezesha kuwa na umeme wa uhakika kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za kilimo.

Meneja Miradi ya Nishati wa EU, Mhandisi Francis Songela amesema katika Mradi huo wamechangia shilingi bilioni 18 na Serikali ya Tanzania imetoa shilingi bilioni 7.

Amesema kituo hicho kipo katika eneo la kimkakati la Mpango wa Kukuza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania , SAGCOT ambapo Mradi huo unaenda kuleta mapinduzi ya kilimo na viwanda.

“Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi ni maeneo ya kimkakati ya SAGCOT kwani yana rutuba kwa kilimo na shughuli nyingi za kiuchumi ambapo umeme wa uhakika ilikuwa changamoto na kwa kuwashwa kwa kituo hiki tunategemea mapinduzi ya kilimo na viwanda, ” amesema Mhandisi Songela.

About the author

mzalendoeditor