Na. WAF – Tanga
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga mjini amekabidhi vifaa vyenye thamani ya Tsh: Mil. 156 ambavyo vinalenga kuharakisha uponaji wa waraibu ambao wamepata nafuu baada ya kuacha kutumia madawa ya kulevya ili kuwawezesha kupata ujuzi wa kufanya kazi za ujasiliamali na kujitegemea.
Waziri Ummy amekabidhi vifaa hivyo leo Novemba 23, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Bombo) kwa Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye naye atakabidhi kwa walengwa ambapo amesema kuwa vijana wakitumia fursa hii vizuri wataweza kushiriki katika kazi za uzalishaji mali na kuaminika kwenye jamii.
Miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa na Waziri Ummy ni pamoja na kits za aluminium zenye thamani ya shilingi milioni 38, vyerehani 10 vyenye thamani ya shilingi milioni 48, mashine mbili za tofali zenye thamani ya shilingi milioni 70.
“Vifaa hivi vinalenga kuharakisha uponaji wa waraibu ambao wamepata nafuu ili kuwawezesha kupata ujuzi wa kufanya kazi za ujasiliamali, kujitegemea na kuinua kipato cha vijana na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema Katika awamu ijayo vifaa vya kuoshea magari (car wash) vyenye thamani ya shilingi milioni 90 vitakabidhiwa katika vituo vya Bombo, Mount Meru na Itega, na vifaa vya saloon za kike na kiume vyenye thamani ya shilingi milioni 61.9 vitakabidhiwa mnamo Desemba, 2023.
“Vifaa ninavyokabidhi leo vinathamani ya Milioni Mia Moja na Hamsini na Sita (Tsh. Mil 156) na vifaa hivyo vitakavyo kabidhiwa awamu ijayo vitakua na thamani ya takribani milioni mia nne na ishirini na tano (Tsh. Mil 425).” Amesema Waziri Ummy
Mwisho, Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali Watanzania katika kuboresha na kuimarisha huduma za Afya pamoja na Wadau katika Sekta ya Afya kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma za Afya hapa Nchini. Aidha amewataka vijana kujiepusha kutumia madawa ya kulevya na wale ambao wanatumia basi waende kujiandikisha kwenye vituo ili kupata huduma za matibabu ambayo yanatolewa bure na Serikali