Featured Kitaifa

SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA RASILIMALI WATU KATIKA SEKTA YA AFYA

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jing,akizungumza  wakati akifungua Mkutano wa 23 wa mwaka wa kitaalam wa mapitio ya mafanikio na changamoto katika sekta ya afya unaoendelea jijini Dodoma.

Na WAF – Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja asasi za kiraia imepanga kuendelea kumiarisha rasilimali watu katika sekta ya afya kwa kuajiri watumishi na kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika kufikisha huduma za afya kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo 23 Novemba 2023 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu wakati akifungua Mkutano wa 23 wa mwaka wa kitaalam wa mapitio ya mafanikio na changamoto katika sekta ya afya unaoendelea jijini Dodoma.

Dkt. Jingu amesema rasilimali watu ndiyo watendaji wakuu wa sekta ya afya hivyo mkutano huo umelenga kujadili upatikanaji wao sehemu ambapo kuna mapungufu lakini pia kuangalia namna ya kuwawezesha kufanya kazi kwa uadilifu wanapokua kwenye maeneo yao ya kazi.

“Uwepo wa rasilimali watu wa kutosha unaenda sambamba na utayari wa kukabiliana na changamoto pale zinapojitokeza hivyo tunataka tujenge utayari wetu wa kutosha ili majanga yanapoingia nchini yakute tukiwa tumejikamilisha”. Amesema Dkt. Jingu.

Aidha, Dkt. Jingu ameongeza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza vya kutosha kwenye sekta ya afya ambapo miundombinu ya afya imejengwa maeneo mengi nchini, hivyo Serikali ina wajibu wa kuhakikisha huduma za afya zinapatikana katika maeneo hayo kwa kupeleka vifaa tiba pamoja na watumishi wenye ujuzi na weledi wa kutosha.

Katibu mkuu huyo ameongeza kuwa katika Mkutano huo utajadili mafanikio na changamoto zilizopatikana katika kipindi cha mwaka 2021-2022 ili kuendeleza pale palipofanikiwa na kuweka mikakati mathubuti kwenye changamoto zilizojitokeza.

Kwa upande mwingine Dkt. Jingu amesema katika nchi kujiweka tayari na changamoto za afya zinazoweza kujitokeza, Serikali imeamua kuwatumia watumishi wa afya ngazi ya jamii (CHW) kuona nini kinachoendelea katika jamii yao kuweza kuwa chachu katika kuhamasisha jamii kushughulikia changamoto zilizopo katika maeneo yao.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Wilson Mahela amesema Mkutano huo ni muhimu wa kujifanyia tathmini ya utoaji huduma katika Vituo vya kutolea huduma kuanzia ngazi ya msingi mpaka Taifa kuonyesha mafanikio na changamoto zilizoibuka.

About the author

mzalendoeditor