Featured Kitaifa

KAMATI YA MAWASILIANO SMZ YAKOSHWA MABORESHO YA MIUNDOMBINU BARA

Written by mzalendo

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ), wakati walipotembelea mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya Usafiri wa Haraka wa Mabasi (BRT), Awamu ya Tatu  Jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Dorothy Ntenga, akitoa taarifa ya Wakala huo kwa wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ), mara baada ya kufika katika Wakala huo, jijini Dar es Salaam.

Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ), wakisikiliza taarifa ya mradi wa Daraja la Tanzanite (km 1.03), kutoka kwa msimamizi wa mradi kutoka TANROADS Eng. Rajab Manger, wakati walipoutembelea mradi huo kwa lengo la kubadilishana uzoefu, Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Efatha Mlav, akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ), wakati walipotembelea mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya Usafiri wa Haraka wa Mabasi (BRT), Awamu ya Tatu Jijini Dar es Salaam

Kazi zikiendelea za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa haraka wa Mabasi (BRT), Awamu ya Tatu inayoanzia katikati ya jiji la Dar es Salaam hadi Gongolamboto ambapo mradi huo umefikia asilimia 20.

…………….

Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imepongeza jitahada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja. 

Pongezi hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Yahya Rashid Abdallah aliyeongozana na wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ), wakati walipofanya ziara ya mafunzo katika Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS). 

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu, hivyo Kamati ikaona ipo haja ya kujifunza na kubadilishana uzoefu baina ya Serikali ya Zanzibar na Tanzania Bara kwenye masuala ya uboreshaji wa miundombinu. 

“Tumeona tuje tujifunze kutoka kwenu, tumeona kazi kubwa iliyofanyika chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yale mazuri tutayachukua na kuyapeleka”, alisema Mhe. Abdallah. 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, alisema ujenzi wa miundombinu nchini ni muhimu kwa kuwa unachochea uchumi na kuongeza fursa za biashara kwa nchi jirani. 

Awali akitoa taarifa ya Wakala huo, Kaimu Meneja wa TANROADS Eng. Dorothy Ntenga, alieleza kuwa Wakala unasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 11,966.38, mizani za kupima uzito wa magari 76 na madaraja 3, 139 katika barabara kuu na zile za mikoa. 

Aidha, ameeleza Wakala huo umekamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege saba na unaendelea na usimamizi wa utekelezaji wa ujenzi wa viwanja vingine tisa. 

Akizungumza baada ya kutembelea mradi wa mabasi yaendayo haraka ya Awamu ya Tatu (BRT III), Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu kutoka TANROADS, Eng. Efatha Mlav, alisema barabara zinazojengwa zinazingatia viwango, ambapo zinaweza kudumu kwa zaidi ya miaka hamsini. 

Alisema kumekuwa na changamoto ya watu wengi kuharibu na kuingilia miundombinu ya barabara licha ya elimu kutolewa mara kwa mara. 

“Sheria ya mwanzo imeainisha hifadhi ya barabara kila upande ni mita 45, hata baada ya kufanyiwa marekebisho ikawa mita 60, wapo wanaovamia licha ya kuwa elimu kutolewa na alama za mipaka kuwekwa”, alisema Eng. Mlavi. 

Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja na barabara ya mabasi yaendayo haraka BRT awamu ya tatu pamoja na mradi wa Daraja la Tanzanite.

 

About the author

mzalendo