Featured Kitaifa

SERIKALI INAJENGA SHULE MPYA KUTATUA CHANGAMOTO YA WATOTO KUTEMBEA UMBALI MREFU

Written by mzalendo

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akieleza lengo la Serikali kujenga shule mpya wakati mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mputa inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP.

Baadhi ya watendaji na viongozi wa Serikali wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde wakati akizungumza nao mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mputa inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mputa Bw. Godlove Chumi (kushoto) akitoa taarifa ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mputa kwa Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP.

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akielekea kukagua madarasa ya Shule ya Sekondari Mputa ambayo inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP.

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akikagua moja ya madarasa yanayojengwa katika Shule ya Sekondari Mputa kupitia mradi wa SEQUIP.

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akisisitiza jambo kwa mkandarasi mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mputa inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP.

Na: James Mwanamyoto 

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inajenga shule mpya nchini, ili kutatua changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu pamoja na kuondoa msongamano wa wanafunzi darasani.

Dkt. Msonde amesema hayo akiwa wilayani Namtumbo, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Mputa inayojengwa kupitia fedha za mradi wa SEQUIP.

Dkt. Msonde amesema Serikali haijengi shule kwasababu ya kujifurahisha au kumridhisha mtu bali inajenga shule kwa lengo la kuwawezesha watoto wasitembee umbali mrefu kufuata elimu.

“Lengo la Mhe. Rais kujenga shule ni kuwawezesha watoto wa kitanzania wanaoingia sekondari kumaliza masomo bila kisingizio cha umbali ili waondoke na ujuzi na umahiri wa kujiletea maendeleo yao pamoja na kuleta maendeleo ya jamii zao na taifa kwa ujumla,” Dkt. Msonde amesisitiza.

Dkt. Msonde amehimiza kuwa, pindi Mhe. Rais akiongeza fedha za ujenzi wa shule za sekondari, watendaji na viongozi wa kisiasa wajenge shule kwa kuzingatia kigezo cha utatuzi wa changamoto ya umbali na msongamano wa wanafunzi darasani na kwenye mabweni. 

Aidha, Dkt. Msonde ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kwa kuchagua eneo zuri la kujenga Shule ya Sekondari ya Mputa na kuongeza kuwa, ujenzi wake ukikamilika vizuri inaweza kuongezwa adhi ya kuwa na kidato cha tano na cha sita.

Akitoa taarifa ya ujenzi kwa Dkt. Msonde, Mkuu wa Shule hiyo ya Sekondari Mputa Bw. Godlove Chumi amesema ujenzi umefikia asilimia 71 na mafundi wanaendelea kujenga giblo, kupiga plasta, blundering, kufunga gypsum board, kupiga koplo, kupachika fremu za mirango na skimming.

Kwa niaba ya bodi ya shule, Kamati ya Ujenzi, Viongozi na Jumuiya nzima ya Kata ya Mputa, Bw. Chumi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kuleta fedha ambazo zinajenga miundombinu ya shule ya Sekondari Mputa.

Kiasi cha shilingi 560,552,827/= kimetolewa na Serikali kupitia mradi wa SEQUIP kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari MPUTA, mpaka sasa kiasi kilichotumika katika ujenzi ni shilingi 379,932,683/= na kiasi kilichosalia kwa ajili ya kukamilisha ujenzi ni shilingi 180,620,144/=.

About the author

mzalendo