Featured Kitaifa

WIZARA ZAASWA KUSHIRIKIANA KUMSIMAMIA MKANDARASI UJENZI BANDARI YA UVUVI LINDI

Written by mzalendo
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso amezitaka Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana kumsimamia mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa bandari ya Uvuvi iliyopo Kilwa Masoko Mkoani Lindi ili ukamilike kwa wakati na viwango.
 
Ameyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mindombinu ya kutembelea na kukagua miradi inayosimamiwa na Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Nchini TPA Kwa bandari ya Kilwa Masoko Tarehe 12 Septemba,2023

 

 

Mwenyekiti Kakoso amesema miradi mingi ya Serikali imekuwa na changamoto ya kutosimamiwa vizuri wakati wa utekelezwaji wake na kuisababishia Serikali hasara mara baada ya miradi hiyo kukamilika na kuzitaka Wizara hizo kuweka mipango Madhubuti ya ukaguzi wa mara kwa mara wa mradi.
“Serikali inatoa fedha nyingi katika kutekeleza miradi ya maendeleo lakini changamoto iliyopo wakandarasi wanaotekeleza miradi hii hawasimamiwi kwa karibu sasa nyinyi mna wataalam wa kutosha waleteni hapa wakague kazi zinazoendelea kila siku tunataka kuona thamani ya fedha zilizowekezwa hapa na viwango pia’ amesema Mwenyekiti Kakoso.
 
 
Kakoso amesema pamoja na ujenzi huo Wizara hizo zihakikishe miradi ya kurejesha kwa jamii (Corporate Social Responsibility) iliyopangwa kutekelezwa inazingatia mahitaji ya wahusika ili wananchi wapate manufaa zaidi kwenye maeneo nje ya uwekezaji huo wa bandari.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile amesema kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha wavuvi kufanya biashara kwa urahisi kwani umezingatia mahitaji yote ikiwemo miundombinu ya kutunzia na kuhifandhi bidhaa za Samaki kabla ya kusafirishwa kwa watumiaji wa ndani na nje ya Nchi.

 

 

 

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Juma Kijavara amemuhakikishia Mwenyekiti Kakoso tayari TPA imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwenye mkataba.

 

 

 

Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Wilayani Kilwa unatekelezwa na Kampuni ya China Harbour Engineering Unaogharimu kiasi cha shilingi bilion 250 ujenzi wake umefikia asilimia 31 na unatarajiwa kukamilika Februari, 2025 ambapo kukamilika kwake kutaifanya Tanzania kuwa na Bandari ya kwanza ya uvuvi ambayo itakuwa kichocheo cha uchumi, kuongeza ajira na upatikanaji wa Samaki wa lishe na kuongeza mapato ya Serikali.

About the author

mzalendo