Featured Kitaifa

EPUKENI VISHAWISHI, CHIPSI NI CHAKULA KAMA VYAKULA VINGINE – WAZIRI UMMY

Written by mzalendo

Na. WAF – Tanga

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka vijana wenye rika balehe (hasa wasichana) kuepuka vishawishi kama chipsi na vingine ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Waziri Ummy ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini amesema hayo leo wakati akifunga kampeni ya Jikubali katika viwanja vya Usagala, Halmashauri ya Jiji la Tanga ikiwa ni tayari imeshazifikia Halmashauri 18 za MIkoa mbalimbali ikiwemo Dodoma.

“Wanangu, njia za kupata maambuzi ya VVU na UKIMWI zipo nyingi lakini epukeni vishawishi kama chipsi kwa kuwa chipsi ni chakula Kama vyakula vingine, tusikubali kudaganyika kwa vishawishi vyovyote vile.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga kutokomeza VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030 ambapo imelenga kuwa na Sifuri Tatu katika maeneo ya maambukizi mapya, vifo na unyanyapaa.

“Kampeni hii ya JIKUBALI itatusaidia kwa kiwango kikubwa kama nchi kufikia malengo makuu ya kutokomeza VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030 ambapo tumelenga kuwa na sifuri tatu katika maeneo ya maambukizi mapya, vifo na unyanyapaa.” Amesema Waziri Ummy

Wazir Ummy ameongeza kuwa takwimu za utafiti wa viashiria vya UKIMWI nchini iliyofanyika mwaka 2016-2017 zinaonyesha hali ya maambukizi iko juu zaidi kwa vijana wa kike, ukilinganisha na wa kiume.

Amesema, kwa vijana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 14, asilimia 0.3 wa kike na asilimia 0.3 wa kiume wanaishi na maambukizi ya VVU, wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19 wa kike ni asilimia 1.0 na wakiume ni asilimia 0.4 na kwa wale wenye umri kati ya miaka 20 hadi 24 wa kike ni asilimia 3.4 wa kiume ni asilimia 0.9.

“Hali hii ya maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa vijana inatuamsha kama Serikali kubuni afua mahususi za kinga zinazolenga kundi hili la vijana rika balehe (hasa wa kike), ikiwemo utoaji wa elimu ya VVU na UKIMWI kwa njia ya Elimu Burudani (edutainment) kupitia watu maarufu na wasanii wenye wasifu wa kushawishi ili kuleta mabadiliko chanya ya tabia hatarishi kwa maambukizi ya VVU miongoni mwa vijana rika balehe mashuleni, ambayo imetuonesha mafanikio makubwa sana”. Amesema Waziri Ummy

About the author

mzalendo