Featured Kitaifa

TFS MBIONI KUANZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUIMARISHA MISITU YA ASILI

Written by mzalendo

 

Mkuu wa Chuo cha Misitu Olmotonyi, Dkt. Joseph Makero amefungua kikao cha awali cha wataalam kuhusu mradi wa “Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuai ya Misitu ya Mazingira Asilia Tanzania Dhidi ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi”  Oktoba 26, 2023, Jijini Arusha.

Mradi huo unaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania – Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS, Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, unalenga  kujenga ustahimilivu wa misitu na bioanuai dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Akifungua kikao kazi hicho Dkt. Makero, aliyekuwa mgeni rasmi amesisitiza umuhimu wa kujenga ustahimilivu wa bioanuai ya misitu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.  

Dkt. Makero anasema mradi huo wa miaka sita una thamani ya Dola za Kimarekani 5.8 milioni utatekelezwa kwa katika misitu tisa ya hifadhi za mazingira asilia nchini Tanzania ikiwemo Mlima Hanang, Nou na Hasama mkoani Manyara, Pindiro, Rondo (Lindi), Uzigua na Pugu Kazimzumbwi (Pwani), Essimingor (Arusha) na Mwambesi mkoani Ruvuma.

“kikao kimefanyika kwa lengo la kujenga uelewa miongoni mwa wataalamu kuhusu malengo na utekelezaji wa mradi huo, na ni hatua muhimu kuelekea kufanikisha juhudi za kuimarisha ustahimilivu wa bioanuai ya misitu nchini Tanzania” alisema Dkt. Makero

Ili kufikia malengo hayo, Dkt. Makero anasisitiza umuhimu wa kushirikiana na wadau kutangaza utalii ikolojia na kufanya maendeleo katika uhifadhi wa bioanuai na ustahimilivu wa mazingira, huku akitoa wito kwa wadau kutumia fursa licha ya changamoto za uhifadhi na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi TFS Prof. Dos Santos Silayo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Zainabu Bungwa ameonyesha utambuzi wa mafanikio ya miradi ya awali kati ya UNDP na Serikali, hasa katika kuboresha hifadhi za mazingira asilia na kuongeza idadi ya watalii na mapato nchini na kuahidi kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, alitoa shukrani kwa UNDP, TAMISEMI na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kazi yao katika kuwezesha mradi huu na kuthibitisha kuwa kushirikiana na UNDP katika miradi ya aina hio kumesaidia kuboresha hifadhi ya mazingira asilia nchini, kuongeza idadi ya watalii, na kuongeza mapato.

Amon Manyama ni Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa UNDP anasema ili kufikia malengo ya mradi huo watendaji wahakikishe wanatumia tekinolojia hususan matumizi ya mitandao ya kijamiii ili kuweza kulifikia kundi kubwa la vijana na makundi mengine maalum katika kuendana na hali ya dunia ya sasa.

Awali akitoa wasilisho la andiko la mradi, Someni Mteleka ambaye ni Mratibu wa Mradi alieleza chimbuko la mradi huo kuwa ni matishio yanayo onekana katika misitu ambayo yanatokana na shughuli za kibinadamu pamoja na ongezeko la idadi ya watu. Aidha, maeneo mengine yalieyoelezwa katika wasilisho hilo ni wadau muhimu katika kutekeleza mradi, jinsi utakavyotekelezwa na namna malengo na matokeo yanayotarajiwa yatasimamiwa kikamilifu ili kufanikisha mradi.

About the author

mzalendo