Featured Kitaifa

KAMATI YA TAMISEMI YARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI WA MIRADI YA ELIMU- SINGIDA

Written by mzalendo

Na.Asila Twaha, Singida

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeridhishwa na hatua iliyofikia ya ujenzi wa shule mpya kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na mradi wa kuboresha elimu ya Awali na Msingi (BOOST).

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 27, 2023 wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Mkoa wa Singida ya kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa kupitia mradi wa SEQUIP na BOOST.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Justin Nyamoga(Mb) amesema, wakiwa ni wawakilishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanafarijika kuona fedha zinazopitishwa na bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinatumiwa kwa matumizi yaliyokusudiwa na kwa kuzingatiwa thamani ya fedha iliyotewa.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo Mhe. Nyamoga ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Singida kwa usimamizi mzuri wa fedha kiasi cha shilingi milioni 544 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Nkuhimtaturu ilipo kata ya Ikungi Halmashauri ya Ikungi na ujenzi wake kufikia asilimia 95.

Amesema, kukamilika kwa shule hiyo ni dhahiri kuwa itasaidia kupunguza changamoto nyingi ikiwemo umbali wa kutembea muda mrefu kwa watoto lakini pia itapunguza kukaa kwa mrundikano kwa wanafunzi madarasani.

” Kwa niaba ya kamati hii, tunamshukuru sana Rais Mhe. Dkt. Samia Suluh Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu kwa maslahi ya nchi yetu” Mhe. Nyamoga

Kwa upande wa ujenzi wa shule mpya ya Msingi Imbele iliyojengwa kupitia mradi BOOST iliyogharimu shilingi mil. 493 iliopo Halmashauri ya Manispaa ya Singida Mhe. Nyamoga amesema, kipindi cha zamani ilikuwa kila mzazi anataka kumpeleka mtoto wake shule za kulipia(private) kutoka na mazingira lakini sasa uwepo wa mazingira mazuri katika shule zetu za Serikali wazazi wengi wanapeleka watoto katika shule za Serikali hivyo, ni jukumu letu kwa pamoja kama wazazi kuhimiza watoto wetu kwenda shule kusoma lakini pia kuwa walinzi na kuitunza miundombinu ya shule ambayo Serikali imetumia gharama kubwa kuijenga.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde ameishukuru Kamati hiyo na kuiahidi yale yote walioyaelekeza na kutoa ushauri wataendelea kuyafanyia kazi na kuieleza kamati hiyo kuwa, taswira walioiona kwa miradi ya elimu katika Halmashauri ya Ikungi na Manispaa ya Singida.

Amesema kupitia mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na Elimu ya Msingi (BOOST )Serikali inaendelea kujenga shule nyengine mpya katika Halmashauri zote 184.

Naye Afisa Elimu Mkoa Singida Dkt. Elpidius Baganda amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Mkoa wa Singida ulipokea fedha kutoka mradi wa BOOST kwa ajili ya ununuzi wa samani na ujenzi wa shule mpya 12 za msingi na kwa upande wa mradi wa SEQUIP tsh.bil 6.3 zilipokelewa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya wasichana ya sayansi na shule mpya 8 za sekondari za kata.

Aidha, Kamati ya TAMISEMI imeutaka uongozi wa Mkoa wa Singida kushirikiana na Mamlaka ya Maji Singida, Tanesco na TARURA kushugulikia changamoto za za kukosekana kwa huduma ya maji, umeme na barabara katika shule ya sekondari mpya iliyojengwa Ikungi na kuhakikisha huduma hizo zinafika kabla ya wanafunzi kufungua shule Januari, mwakani.

About the author

mzalendo