Featured Kitaifa

DKT. NCHEMBA AIAGIZA PPRA KUUNGANISHA MFUMO WA GIMIS NA NeST

Written by mzalendo

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa GIMIS na majengo mapya ya Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA), katika hafla iliyofanyika katika ofisi za Wizara ya Fedha ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri wa GPSA, Bi. Dorothy Mwanyika, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dr. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu Utumishi. Bw. Juma Selemani Mkomi akifuatiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa GPSA, Prof. Geraldine Rasheli.

Na. Farida Ramadhani, Saidina Msangi, WF, Dodoma

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuhakikisha inaunganisha Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) na Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki katika Utoaji wa Huduma za Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GIMIS) ili kurahisisha mchakato wa ununuzi Serikalini.

Waziri Nchemba akitoa maelekezo hayo wakati akizindua wa Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki katika Utoaji wa Huduma za Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini ujulikanao kama GIMIS (GPSA Intergrated Management Informationm System), uliofanyika katika katika Ukumbi wa Kambarage, Hazina Jijini Dodoma.

Alisema PPRA iunganishe mifumo hiyo haraka iwezekanavyo kwa kuwa Mfumo wa GIMIS unatumiwa na Wizara, Mashirika ya Umma, Wakala, Ofisi za mikoa na Halmashauri za Wilaya nchini katika kupata huduma za GPSA.

“Mhe. Rais – Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mifumo ya Serikali isomane hivyo ni muhimu mifumo mingine ihakikishe inaunganishwa na GIMIS ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini” alibainisha Mhe. Nchemba.

Alisema kuwa Mfumo wa GIMIS utaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini kwa kuwa majukumu yote ya Wakala yanatekelezwa ndani ya mfumo huo.

Aidha, Dkt. Nchemba alitoa wito kwa Taasisi nunuzi kuhakikisha wanatumia huduma za GPSA kwa kuwa Sheria ya Ununuzi na Kanuni zake inazitaka kupata huduma na vifaa mtambuka kupita GPSA.

Aliipongeza GPSA kwa kukamilisha ujenzi wa mfumo huo na majengo ya ofisi na vituo vipya vya mafuta vya Songwe, Simiyu, Pwani na Dodoma pamoja na kufanya ukarabati katika ofisi za mikoa 17 na kusimika matenki ya mafuta katika mikoa 12, kwa kuwa hatua hiyo itaongeza mapato na morali ya utendaji kazi kwa watumishi.

Mhe. Nchemba pia aliipongeza GPSA kwa kuendelea kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo katika kipindi cha miaka mitano mpaka kufikia mwaka 2022/2023 imechangia kiasi cha Sh. bilioni 11.9.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alisema mfumo huo umeshaunganishwa na Mfumo Mkuu wa Serikali ambao unaiwezesha mifumo kubadilishana taarifa na umeshaanza kubadilishana taarifa na baadhi ya mifumo ya taasisi za umma ikiwemo Mfumo wa Kukusanya Mapato ya Serikali (GePG) na Mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali za Serikali.

Aliongeza kuwa jitihada zinaendelea kuunganisha Mfumo huo na mifumo mingine ya Serikali kulingana na mahitaji ya ubadilishaji wa taarifa na kubainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kisheria yatawezesha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kusimamia masuala ya Serikali Mtandao kwa ufanisi.

Aidha, aliziasa taasisi nyengine za umma ambazo bado zinakiwango kidogo cha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kuongeza juhudi katika matumizi ya tehama katika utekelezaji majukumu yao kama Sheria ya Serikali Mtandao inavyoelekeza.

“Ni wajibu wa kila taasisi kuweka jitihada za makusudi ili kuhakikisha zinafaidika na fursa zinazotokana na matumizi ya tehama ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kutimiza adhma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuelekea katika Serikali ya Kidigitali”, alibainisha Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri GPSA, Bi. Dorothy Mwanyika alisema kuwa mfumo huo utatoa huduma katika ununuzi wa vifaa vya ofisi, mafuta katika vyombo vya moto, huduma ya ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali katika maeneo ya bandarini, viwanja vya ndege na mipakani.

Alibanisha kuwa mfumo huu utatumika katika huduma ya ununuzi wa magari ya Serikali ikijumuisha kuanzia maombi ya vigezo, kibali cha ununuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, utoaji wa hati za madai ya ununuzi wa chombo husika pamoja na kuwezesha uombaji wa kibali cha usajili kutoka Wizara ya Fedha na usajili wa chombo cha moto husika utakaofanywa na Wizara ya ujenzi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa majengo mapya ya Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA) yaliyoko katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dr. Natu El-maamry Mwamba na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri GPSA Bi. Dorothy Mwanyika.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb) wakishuhudia mfumo wa GIMIS unavyofanyakazi baada ya kuzinduliwa rasmi katika hafla iliyofanyika katika ofisi za Wizara ya Fedha ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akipokea Tuzo kwa niaba ya Mhe. Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb). Mhe. Rais ametunukiwa tuzo hiyo ya Shukrani kwa kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya mifumo ya Tehama ikiwemo Mfumo wa GIMIS katika hafla ya ya uzinduzi wa Mfumo huo na majengo mapya ya Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA), katika hafla iliyofanyika katika ofisi za Wizara ya Fedha ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa GIMIS na majengo mapya ya Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA), katika hafla iliyofanyika katika ofisi za Wizara ya Fedha ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri wa GPSA, Bi. Dorothy Mwanyika, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dr. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu Utumishi. Bw. Juma Selemani Mkomi akifuatiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa GPSA, Prof. Geraldine Rasheli.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb), akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa GIMIS na majengo mapya ya Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA), katika hafla iliyofanyika katika ofisi za Wizara ya Fedha ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.

Meza kuu ikiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA), baada ya kuzinduliwa kwa Mfumo wa GIMIS na majengo mapya ya GPSA, katika hafla iliyofanyika katika ofisi za Wizara ya Fedha ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dr. Natu El-maamry Mwamba. Kulia kwake ni Mwenyekiti Bodi ya Ushauri GPSA, Bi. Dorothy Mwanyika na Ofisa Mtendaji Mkuu wa GPSA, Prof. Geraldine Rasheli.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)

About the author

mzalendo