Featured Kitaifa

BMH KUANZA KUTOA MATIBABU YA MOYO BILA KUFUNGUA KIFUA KWA WATU WAZIMA

Written by mzalendoeditor

 

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Oktoba 10,2023 jijini Dodoma kuelekea Miaka nane ya utoaji wa huduma katika hospitali hiyo.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya damu  ambaye ameshinda  tuzo ya daktari bora wa mwaka wa Dk. Stella Malangahe ,akitoa shukrani kwa uongozi wa hospitali hiyo pamoja na  serikali kwa ujumla kutokana na kuwekeza katika suala la sekta ya afya katika Hospitali hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika,akimkabidhi Tuzo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya damu  ambaye ameshinda  tuzo ya daktari bora wa mwaka  Dk. Stella Malangahe hafla iliyofanyika  leo Oktoba 10,2023 jijini Dodoma kuelekea Miaka nane ya utoaji wa huduma katika hospitali hiyo.

Na.Alex Sonna-DODOMA

KATIKA Kuelekea Miaka nane ya utoaji wa Huduma Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa imetangaza kuanza kutoa huduma ya upasuaji wa moyo bila kufungua kifua kwa watu wazima ambayo inatarajia kuanza Oktoba 16, mwaka huu.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 10,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Dkt. Alphonce Chandika amesema mafanikio yote yanatokana na kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma.

 Dk. Chandika, amesema kuwa lengo la kuanza kutoa huduma hiyo ni kuipunguzia mzigo Taasisi ya Matibabu ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo inayopokea wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

“Kambi ya madaktari bingwa inatarajia kuanza Oktoba 16, 2023 hapa hospitalini, awali hospitali ilikuwa ikitoa matibabu haya kwa watoto wadogo na kuwapa rufaa watu wazima kwenda Jakaya Kikwete,”amesema Dkt.Chandika

Aidha amesema kuwa wameamua  kuanzisha matibabu ya aina hiyo ili  kuokoa maisha ya watu wenye tatizo hilo ili kuwapunguzia gharama wananchi kutoka Dodoma kwenda Dar es salaam lakini na kuipunguzia msongamano Taasisi ya Kikwete.

Hata hivyo amesema wanajivunia utoaji wa huduma bora za kibingwa ikiwemo upasuaji wa huduma ya nyonga na magoti ambapo zaidi ya wananchi 100 wamepata huduma hiyo.

”Utoaji wa huduma hizo umesaidia kupunguza gharama ya kwenda kutibiwa nje yanchi,umepunguza muda wa mtu kupata matibabu na kupunguza idadi ya watu wanaopata kilema na wengine kufariki kutokana na kuchelewa kupata huduma kwa wakati.”amesema Dkt.Chandika

Aidha katika Miaka nane ya utoaji wa huduma imejidhihirisha katika utoaji wa huduma bora ambapo mtumishi wa hospitali hiyo Dkt.Stellah Malangahe amepewa tuzo ya kuwa daktari bora wa mwaka ambaye anaushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa ushirikiano.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya damu  ambaye ameshinda  tuzo ya daktari bora wa mwaka wa Dk. Stella Malangahe amesema kuwa ushindi huo  umeipa heshima kubwa hospitali hiyo na kuishukuru serikali kutokana na kuwekeza katika sekta ya afya.

“Naishukuru sana serikali kwa ujumla kutokana na kuwekeza katika suala la sekta ya afya, huduma hizi bora zinakuja kutokana na vifaa vya matibabu vinavyotolewa katika hospitali mbalimbali hapa
nchini,”amesema Dk. Malangahe

Hospitali ya Benjamin Mkapa ilizinduliwa rasmi Octoba 13 mwaka 2015 ambapo kuanzishwa kwake imekuwa ni mkombozi kwa Taifa dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo husababisha vifo vingi.

About the author

mzalendoeditor