Featured Kitaifa

SERIKALI  KUZINDUA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA UTAMBUZI WA SHUGHULI ZA NGOs

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Septemba 27, 2023  kuelekea Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakalofanyika Oktoba 03 hadi 05, 2023 jijini Dodoma.

Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs), Bi.Vickness Mayao,akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Septemba 27, 2023  kuelekea Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakalofanyika Oktoba 03 hadi 05, 2023 jijini Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza na  waandishi wa Habari  kuelekea Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakalofanyika Oktoba 03 hadi 05, 2023 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI ya inatarajiwa kuzindua mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama Ramani ya Didigitali ya utambuzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali utakaokwenda kudhibiti utendaji kazi wa mashirika yasiyofuata sheria na kanuni za usajili na uendeshaji wa mashirika hayo nchini.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 27,2023 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na waandishi wa Habari  kuelekea Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakalofanyika Oktoba 03 hadi 05, 2023 jijini Dodoma
Dkt. Gwajima amesema  jitihada za Serikali ni kutengeneza Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kukabiliana na changamoto ya kiutendaji  ya Mashirika hayo na utekelezaji wa miradi na afua zinazofanana ndani ya eneo moja.
“Wizara kwa kushirikiana na wadau iliamua kuboresha  Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuongeza Ramani ya Utambuzi wa Mashirika kwa njia ya kidijitali ambapo ramani itasaidia Wadau, Taasisi za Kiserikali, Sekta Binafsi na Jamii kupata taarifa za Mashirika kwa urahisi.” amesema Mhe. Gwajima.
Hata hivyo ametaja  faida za kuwepo kwa Ramani ya Utambuzi wa Mashirika kwa njia ya kidijitali amesema ni pamoja na kujua mahali au eneo shirika lilipo; kujua eneo la utekelezaji wa miradi ya Mashirika (thematic area),  afua zinazotekelezwa, wanufaika wa mradi,  mchango wa mashirikia upande wa ajira zilizotolewa na Mashirika hayo.
Faida zingine ni kuuliza na kupata majibu ya moja kwa moja kujua fursa zilizopo, kujua Mashirika yaliyokiuka vigezo vya usajili wake, kutambua mchango wa Mashirika kupitia fedha za miradi, kujua idadi ya Mashirika kwenye kila Mkoa, Wilaya na Halmashauri na kujua miradi inayotekelezwa kwa wingi au uchache katika Mikoa.
 “Ramani hii itawezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji ili kuleta maendeleo endelevu nchini na mchango wake kuonekana bayana kwa Maendeleo ya Taifa,” ameongeza Dkt. Gwajima.
Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Gwajima amesema, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) imeandaa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakalofanyika kuanzia tarehe 03 – 05 Oktoba, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini  Dodoma ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
“Lengo kuu la Jukwaa ni kuimarisha Mahusiano baina ya Serikali, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau wengine pamoja na kutambua mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Dkt. Gwajima.
Aidha ameeleza kuwa  mwaka huu, Jukwaa hilo litajumuisha washiriki zaidi ya 2000 huku Kaulimbiu ikiwa ni Mashirika Yetu, Maadili Yetu, Taifa Letu. 
kwa upande wake Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs), Bi.Vickness Mayao, amesema kuwa mpaka sasa zaidi ya mashirika 9900 yamesajiliwa na yanatoa huduma mbalimbali.

About the author

mzalendoeditor