Na Mwandishi Wetu Zanzibar
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amekabidhi mipira ya maji kwa wakazi wa eneo la Mpapa lililopo Wilaya ya Kati ikiwa ni ahadi yake ya kutatua changamoto za upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
Naibu Waziri Mwanaidi, amekabidhi mipira hiyo mapema Septemba 26, 2023 ambapo aliambatana na Naibu Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga huku akiwaeleza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati kuendelea kutatua changamoto mbalimbali katika jamii ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu ikiwemo ya maji.
“Niliahidi wakati wa ziara yangu, hii leo naitimiza kwa kukabidhi mipira hii, ili kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji, niwatakie kila lenye kheri katika kutunza mipira hii na endeleni kuiunga mkono Serikali yetu yenye nia dhabiti katika kuhakikisha uwepo wa huduma muhimu za kijamii,” amesema Mhe. Mwanaidi
Aliongezea kuwa, hii ni sehemu ya kuunga jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani na kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi kwa kuondokana na changamoto zinazoweza kuwakwamisha katika utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera,Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga aliwakumbusha wakazi hao kuitunza mipira hiyo pamoja na kuwasihi kushirikiana kwa umoja katika masuala mbalimbali ya maendeleo nchini.
Naye Diwani wa Viti Maalum Wilaya ya Kati Mhe. Khadija Kassim akitoa shukrani kwa Naibu Waziri huyo alisema wamefarijika na kuendelea kuipongeza Serikali kwa kutatua changamoto zinazowakabili huku akitoa neno kwa wakazi hao kuunga mkono juhudi za Serikali yao.
“Binafsi naendelea kumpongeza sana Naibu Waziri Mwanaidi kuona umuhimu na kutuvusha katika hili, hii imekuwa historia kwetu, tunaona jitihada hizi kwa matendo siyo kwa huduma za maji tu, hata masuala ya afya, nishati na nyingine nyingi.”amesema Mhe. Khadija