Featured Kitaifa

MBUNGE MTATURU ALIPIGA JEKI KANISA

Written by mzalendoeditor

 

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amechangia Sh Milioni tatu katika harambee ya ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Ikungi huku akilipongeza Kanisa kwa kuendelea kuiombea amani nchi.

Kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya ununuzi wa saruji mifuko 50,nondo za Sh Milioni moja,matofali 300 na gharama ya kumlipa fundi Sh 600,000 ambapo mbali na hayo ameahidi pia kutoa pikipiki moja ili kusaidia kwenye kazi ya utume kanisani hapo.

Akichangia harambee hiyo Septemba 24,2023,kanisani hapo,Mtaturu amesema serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaleta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Miradi hiyo ipo katika sekta ya afya,maji,umeme,elimu na barabara,miradi hii inaletewa fedha nyingi kwa ajili yetu hivyo ni jukumu letu kuendelea kumuombea Rais wetu na kuiunga mkono serikali yetu,”amesema.

Awali Paroko Padre Vincent Alute amemshukuru sana mbunge huyo kwa kwenda kushiriki nao ibada na kuwaunga mkono kwenye harambee ya ujenzi wa kanisa jipya uliofikia usawa wa madirisha.

“Sisi tumefarijika sana na ujio wako hii leo,lengo letu hapa ni kupata Sh Milioni 10 ili tukamilishe ujenzi huu,lakini kupitia mchango wako Mbunge wetu utaenda kutusogeza kwa kiasi kikubwa,tukuahidi kuwa tutaendelea kumuombea Rais wetu na serikali yake kwa ujumla ili iendelee kukidhi matamanio ya wananchi,”amesema.

About the author

mzalendoeditor