Featured Kitaifa

TANI 370 ZENYE THAMANI YA SH .BILIONI 741.5 ZAUZWA KUPITIA MFUMO STAKABADHI GHALA

Written by mzalendoeditor

 

KAIMU Mkurugenzi Mtendaji, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala Bw.Asangye Bangu, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Taasisi hiyo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.

Na.Alex Sonna-DODOMA

BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala inaendelea na uhamasishaji kwa wananchi juu ya faida za matumizi ya mfumo huo mpaka kufikia Juni 30 mwaka 2022/2023 jumla ya mazao 13 ikiwemo Soya na Mbaazi yenye tani 370 zenye thamani ya Sh bilioni 741.5 zimeuzwa kupitia mfumo huu.

Hayo ameyasema leo Agosti 16,2023 jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala Bw.Asangye Bangu, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Taasisi hiyo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.

Bw.Bangu amesema kuwa hadi  kufikia Juni 30 mwaka huu jumla ya mazao 13 ikiwemo Soya,Mbaazi,Ufuta,Dengu,Korosho yameweza kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala hapa nchini ambapo kiasi cha kilogram 370,766, 931 (sawa na tani 370.7) zenye wastani wa thamani ya Sh 741,533,862,000.00 (kwa kuchukua bei ya wastani ya shilingi 2000 kwa kilo) zimeuzwa kwa njia ya mnada katika mwaka wa fedha wa 2022/23 na kuwafikia Watanzania, hususan wakulima.

Pia amesema kuwa  kiasi hicho cha mazao kumewezesha takriban kiasi Sh 22,246,015,860.00 kupelekwa serikalini kupitia halmashauri zao.

“Hii ikiwa imehusisha mikoa iliyotekeleza Mfumo peke yake.”

”Mfumo wa stakabadhi za ghala zimechangia ongezeko la bei ambapo kwa zao la Kakao, kutoka watasani wa Sh 500 kwa kilo hadi kufikia Sh 7,739, huku kwa zao la ufuta limetoka Sh 800 hadi kufikia Sh 4,000 kwa kilo wakati kwenye zao la kahawa imeongezeka kutoka Sh 1,000 kwa kilo hadi kufikia Sh 3,700 kwa kilo.”amesema Bw.Bangu

Hata hivyo ameeleza kuwa kwa mwaka 2023/24, Bodi imeendelea kupeleka Mfumo katika maeneo ya Kanda zote nchini kwa bidhaa na kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Soko la Bidhaa Tanzania wamekamilisha Mwongozo wa mauzo ya mazao jamii ya Kunde ikiwemo Soya, Dengu, Mbaazi na Choroko.

Mfumo tayari umeanza kutumika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Tanga, Morogoro na Manyara.

 ”Bodi imejipanga kutawanya matumizi ya Mfumo huu katika maeneo mengine na kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mazungumzo na NARCO ili kuona namna ambavyo stakabadhi za ghala inaweza kuchangia kuongeza tija katika Mpango wa “Cattle guest house” kwenye mpango wa Wizara uanohusu usajili, uhifidhi na unenepeshaji wa mifugo.”amesema

Amesema  pia Bodi inaendelea na maandalizi ya kuliingiza zao la Mwani linalozalishwa ukanda wote wa Pwani kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kushirikiana na vyama vikuu vya ushirika katika maeneo hayo.

Aidha amesema kuwa Bodi inaendelea na maandalizi ya kuingiza za asali hususan katika Mkoa wa Tabora, kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Sikonge.

“Hii itasaidia kuleta ushindani wa wanunuzi hivyo kuchochea bei na kuongeza ubora wa zao.”

Amesema  pia Bodi imeingia makubaliano na TANTRADE ili kuweza kusaidia kuhakikisha kuwa wateja wanaopatikana kutoka nje ya nchi wanakusanyiwa bidhaa kwa kuzingatia ubora.

About the author

mzalendoeditor