Featured Kitaifa

TEA KUTUMIA BILIONI 8 KUFADHILI MIRADI YA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA ELIMU NCHINI

Written by mzalendoeditor

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bahati Geuzye,  akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa Fedha 2023/24.

Na.Alex Sonna-DODOMA

KATIKA mwaka wa Fedha 2023/24  Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)  imepanga kutumia Sh Bilioni 8 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu Nchini.

Hayo yamesemwa leo Agosti 10,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bahati Geuzye, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo.

Amesema kuwa wanafunzi 39,484 na walimu 169 wa shule za msingi na sekondari wanatarajia kunufaika na miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini kwenye shule 81.

“Fedha hizi zitatumika kufadhili miradi 82 katika shule 81 zikiwemo za msingi 48 na sekondari 33 zilizopo maeneo mbalimbali ya Tanzania bara,”amesema 

Aidha ameeleza kuwa miradi itakayofadhiliwa ni pamoja ujenzi wa madarasa 82, matundu ya vyoo 336, mabweni 10, ujenzi wa maabara 18 za masomo ya sayansi na nyumba za walimu 32.

Amesema  Mfuko wa Elimu wa Taifa utatoa ufadhili kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na kuwezesha ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika taasisi moja ya elimu ya juu Tanzania Zanziba utakaogharimu sh.milioni 300.

Hata hivyo amesema kuwa  katika mwaka 2018/19 hadi mwaka 2022/23, Sh.Bilioni 20.1 zimetumika katika utekelezaji wa miradi kwenye Taasisi 235 chini ya Mfuko wa kuendeleza Ujuzi.

“Taasisi zilizopata ufadhili zimetekeleza program za mafunzo ya ujuzi kwa vijana katika sekta za kilimo na kilimo uchumi, TEHAMA, utalii na huduma za ukarimu, nishati, ujenzi na uchukuzi,”amesema

Pia amesema kuwa watu 49,063 wamenufaika saw ana asilimia 114 ya walengwa, kati yao wanawake 22,413 sawa na asilimia 46 na wanaume 26,650 sawa na asilimia 54 ya wanufaika wote.

“Vijana walionufaika ni pamoja na vijana 464 waliotoka kundi la watu wenye ulemavu, vijana 2,928 walitoka kundi la vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu kwa upande wa Tanzania Bara na 600 walitoka kundi la vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu walinufaika kwa upande wa Tanzania Zanzibar,”amesema.

About the author

mzalendoeditor