Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri, Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya vijana Duniani (International Youth Day) uliofanyika tarehe 10 Agosti, 2023 jijini Dodoma.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) Majaliwa Marwa akieleza jambo wakati wa mkutano huo kuelekea maadhimisho hayo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Mkoani Dodoma (DOYODO) Rajabu Juma akizungumza jambo wakati wa mkutano huo.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana Agosti 12, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na wadau imeandaa kongamano la kitaifa la vijana litakalofanyika kesho jijini Dodoma.
Akizungumza Agosti 10, 2023 na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof. Jamal Katundu, amesema kongamano hilo litashirikisha vijana 600 ambapo pamoja na mambo mengine vijana watajadili ustawi na maendeleo yao.
Pia, amesema siku ya kilele vijana watashiriki katika shughuli za maonesho na bonanza katika viwanja vya chang’ombe Dodoma na watapatiwa huduma za upimaji wa afya kwa hiari, ushauri nasihi, elimu ya afya ya uzazi pamoja na kujitolea kuchangia damu salama ili kuwasaidia wahitaji katika hospitali nchini.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni ‘Kuelekea 2030: Vijana na Ujuzi wa Mazingira kwa Maendeleo Endelevu’ inayokumbusha jumuiya za kimataifa suala la kulinda na kuhifadhi mazingira.