Featured Kitaifa

WAFUGAJI JIJI LA DODOMA WATAKIWA KUFUGA KISASA

Written by mzalendoeditor

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WAFUGAJI katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kufuga kisasa ng’ombe wachache wenye uwezo mkuwa wa kuzalisha.

Kauli hiyo ilitolewa na Amos Mwamyovellah, Mkurugenzi Mtendaji wa AJM&S Mwamyovellah Farm Production alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliotembelea banda la mifugo la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika maonesho ya Nanenane jijini Dodoma.

Mwamyovellah alisema “ng’ombe hawa tumewaleta katika maonesho haya ya Nanenane ili kuwasaidia wenzetu wafugaji wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuweza kufuga kisasa. Wafugaji wanatakiwa kuwa na ng’ombe wa chache lakini wenye uwezo mkubwa kiuzalishaji”.

Akiongelea chakula kinacholiwa na ng’ombe hao alisema kuwa wanakula chakula kizuri kilichoandaliwa kitaalam. “Chakula hiki kimechanganywa kitaalam kwa kutengeneza lishe bora kwa ng’ombe ili waweze kutupatia maziwa. Ng’ombe hawa tunakamua asubuhi, mchana na jioni kulingana na wingi wa maziwa. Ng’ombe anatoa lita 36 za maziwa na anafika lita 40 akiwa katika mzao wake wa kwanza na sasa ana kilo 780. Kama unavyomuona ni mpole na hana shida wakati wa kukamua” alisema Mwamyovellah.

Alisema kuwa ng’ombe hao wanawapandisha kwa chupa ili kuweza kupata ubora wa ng’ombe. Na mwendelezo wa ng’ombe hawa hivyo tunatumia ‘artificial insemination’. “Ng’ombe huyu ana uwezo wa kuchangia 50% katika uzazi na dume akachangia 50%. Niwaombe wafugaji wenzangu waweze kutembelea banda letu hapa Nanenane Halmashauri ya Jiji la Dodoma tujifunze kwa pamoja tuweze kulima nyasi tuache kuzurura kwa ng’ombe ili tuweze kufuga katika eneo dogo na tuweze kupata uzalishaji mkubwa kulingana na ng’ombe ambao tunawafuga” alisema Mwamyovellah

Mwananchi aliyetembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Juma Alphonce alisema ni mara yake ya kwanza kuona ng’ombe anayetoa maziwa makubwa kiasi hicho. “Haya maonesho yanatusaidia kupata elimu ya ufugaji bora. Niwashauri wananchi wenye nia ya kufuga ng’ombe kutembelea banda hili ili waweze kupata elimu bora ya ufugaji” alisema Alphonce.

Maonesho ya shughuli za wakulima Nanenane mwaka 2023 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula”.

About the author

mzalendoeditor