Featured Kitaifa

RC SENYAMULE AAGIZA CHEMBA KUKAMILISHA MIRADI KWA WAKATI

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule akizungumza na wananchi wa Kata ya Kwa Mtoro katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Agosti 4 katika Kijiji cha kwa Mtoro ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi Wilayani Chemba 

Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma Mwl. Gift Kyando akizungumza na wananchi wa Kata ya Kwa Mtoro katika Mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa kata hiyo. Mkutano huo umefanyika Agosti 5/2023.

Mhe. Senyamule akipokea Taarifa ya mpango kazi wa namna ya utekelezaji wa Mradi wa Shule Mpya ya kata ya Sekondari Babayu wakati alipofanya ziara yake ya kikazi Agosti 4 Mwaka huu ya kukagua Miradi ya Shule za Msingi na Sekondari inayotekelezwa katika Wilaya ya Chemba. 

Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald Mongella akiteta Jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Senyamule wakati wa Mkutano wa Hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kijiji cha Kwa Mtoro

Msafara wa Mkuu wa Mkoa Dodoma katika ziara yake ya kikazi ya kukagua Miradi ya Shule za Msingi na Sekondari inayotekelezwa kupitia fedha za Boost na Sequip Wilayani Chemba, ziara hiyo imefanyika Agosti 4 Mwaka huu.

Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu bora ya elimu katika Mkoa wa Dodoma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Shule mpya za Msingi na Sekondari, ujenzi wa maabara na mabweni katika Wilaya zote zilizopo Mkoani Dodoma.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule kwa nyakati tofauti wilayani Chemba katika ziara yake ya kikazi ya kukagua hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya elimu wilayani humo.

“Ninatembelea Wilaya zenye changamoto ambazo bado hazijakamilisha miradi yake kama ilivyopangwa. Hapa Magugu ujenzi wa hii shule ulitakiwa kukamilika Juni 30, 2023 na leo ni tarehe 3 Agosti, wako katika hatua za ukamilishaji, hata hivyo ujenzi wa choo bado haujakamilika,kazi hizi zilikuwa ziende Pamoja” Senyamule alihoji.

Aidha, ametoa muda wa siku saba  kwa Mkuu wa Shule hiyo kukamilisha ujenzi wa choo ili shule hiyo iweze kuanza kutumika. 

“Tunategemea maelekezo na ushauri vifanyike kwa wakati mmoja,nimeshaelekeza ununuzi wa vifaa vyote ufanyike kwa pamoja kusiwe na ucheleweshaji wa aina yoyote ile na sababu zisizo na msingi.

Katika hatua nyingine Mhe. Senyamule amemwagiza Mwl Mkuu wa Shule hiyo ya Magungu Mwl. Edwin Fredrick kuthaminisha nguvu kazi inayochangiwa na wananchi. 

“Thaminisheni mchango wa wananchi, wapewe taarifa kuwa mchango wao wa nguvu kazi ni shilingi ngapi, ili fedha inayobaki kutokana na mchango wa nguvu za wananchi ziweze kufanya kazi nyingine mfano Ujenzi wa nyumba za walimu.

Pia, ameagiza kukamilishwa kwa ujenzi wa vyoo katika shule hiyo ndani ya wiki moja, huku akiwataka kuongeza kasi katika miradi inayoendelea ya Sequip na Madarasa ya kidato cha Tano.

“Hatuwezi kuwa na mpango wetu kama Mkoa wa kukamilisha miradi ya ujenzi na wewe mwalimu una mpango wako, hii ni kazi ya Serikali, nitarudi ndani ya wiki moja” Senyamule amesisitiza

Mkoa wa Dodoma kupitia mradi wa Boost umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10.6 kwa ajili ujenzi wa Shule mpya 16, vyumba vya madasa ya msingi 163, madarasa ya awali 16, ujenzi wa vyoo 106, nyumba za walimu 03 na darasa 01 la elimu maalumu. Wilaya ya Chemba imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 na Kondoa Mji na Halmashauri Shilingi Bilioni 1.7.

Katika ziara hiyo Mhe. Semnyamule alipata fursa ya kukagua Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Babayu,Shule mpya ya Msingi Magungu, Ujenzi wa mabweni na madarasa katika shule ya Sekondari Msakwalo pamoja na kufanya Mkutano wa kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi katika kata ya kwa mtoro Kijiji cha kwa mtoro.

About the author

mzalendoeditor