Na WMJJWM, DSM
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amemtembelea mwanamke anayejitolea kukumbatia watoto njiti waliotelekezwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana Mariam Mwakabungu ili kuendelea kumtia moyo.
Akizungumza katika wodi ya watoto njiti hospitalini hapo, Mhe. Mwanaidi amesema kuwa lengo ni kumpongeza na kumtia moyo ili kuhakikisha anakuwa na amani katika malezi ya watoto hao.
“Tumekuja katika Hospitali hii ya Amana kumsaidia huyu mama pamoja na kumpongeza na sisi kama Wizara tunaungana na Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuhakikisha mama huyu anaishi vizuri. Lakini pia kuhamasisha kina mama wengine nao watakaposikia jambo kama hili waweze kuja kuwasaidia watoto hawa.
Mhe. Mwanaidi amewataka Maafisa wa Ustawi wa Jamii kupita kila Zahanati kuhakikisha wanaibua changamoto zilizopo na kuziwasilisha Wizarani ili zifanyiwe kazi.
Mwanaidi ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa kufanikisha kumpatia ajira ya mkataba.
Naye Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana, Dk. Bryceson Kiwelu amesema jambo hilo liligunduliwa na wauguzi wa kitengo hicho kwa kushirikiana na madaktari wao.
“Hospital imekuwa ikifanya kazi na makundi mbalimbali ya kijamii, sio tu huyu mama ameibuliwa wapo wengi ambao walikuja kama wafanya usafi na tumeona jinsi ambavyo walifanya vizuri na kupata fursa,” ameeleza Dk. Kiwelu.
Amebainisha kuwa tayari Mariam ameshawasaidia watoto watatu ambapo wawili wanaendelea vizuri na wamepelekwa katika vituo vya kulelea watoto yatima.
“Pamoja na kwamba Waziri Ummy ameagiza apewe ajira ya mkataba, mchakato unaendelea ili aweze kuendelea na masomo ya jioni kwani Mariam aliishia kidato cha pili ili atakapohitimu kidato cha nne aweze kupewa ajira serikalini,” amesema Dk. Kiwelu.
Naye Mariam, ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuutambua mchango wake na kumuunga mkono.
“Nakushukuru pia Naibu Waziri, sina cha kuwalipa zaidi ya kumshukuru Mungu.