Featured Kitaifa

VYAMA VYA USHIRIKA VYASHIRIKISHWA KUSAMBAZA MBOLEA

Written by mzalendoeditor

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) , Dkt. Stephan Ngailo,akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la TFRA wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Dunia,yaliyofanyika Julai Mosi,2023 Mkoani Tabora.

Meneja Mkuu Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Samuel Mshote,akizungumza wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Dunia,yaliyofanyika Julai Mosi,2023 Mkoani Tabora.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe,akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) , Dkt. Stephan Ngailo,mara baada ya kutembelea banda la TFRA wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Dunia,yaliyofanyika Julai Mosi,2023 Mkoani Tabora.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe,akisaini kitabu cha wageni kwenye banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) mara baada ya kutembelea banda hilo  wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Dunia,yaliyofanyika Julai Mosi,2023 Mkoani Tabora.

Na Alex Sonna-TABORA

SERIKALI imetoa bei elekezi ya mbolea ya ruzuku kwa wakulima nchini na kusisitiza mbolea hiyo itanunuliwa karibu na maeneo yao.

 Mpango huo wa ruzuku ulianza kwa mwaka wa fedha 2022/23 na serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa kwa mwaka wa fedha 2023/24 Sh.Bilioni 130 zimetengwa kwa ajili hiyo na bei kama ilivyokuwa kwenye msimu uliopita.

Akizungumza Julai mosi, 2023 mkoani Tabora, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) , Dkt. Stephan Ngailo, amesema bei elekezi ya msimu uliopita inaendelea kutumika ambapo ni Sh.70,000 kwa mbolea ya DAP, UREA, NPKs, Sh.60,000 kwa mbolea ya CAN na Sh.50,000 kwa mbolea ya SA.

Amesema katika kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima, mamlaka imeweka mikakati ya kutumia vyama vya ushirika ambapo hadi sasa zaidi ya 220 vimesajiliwa na mafunzo yametolewa kwa vyama 400 na bado wanaendelea.

Amesema bei hizo zitaanza kutumika kuanzia tarehe 01 Julai, 2023 hadi tarehe 15 Agosti na tofauti kati ya bei elekezi kwa kila eneo na bei ya mkulima italipwa na Serikali kama ruzuku kwa mkulirna kwa lengo la kumpunguzia makali ya bei. Aidha, vifungashio vya ujazo wa kilo tano vitauzwa kwa bei elekezi ya soko.

“Niwatoe hofu wakulima kama serikali ilivyoahidi kwa msimu huu tunakwenda kutekeleza na kuhakikisha zinafika kwa wakati na wakulima ambao hawajajisajili wakajisajili na kuhuwisha taarifa zao,”amesema.

Naye, Meneja Mkuu Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Samuel Mshote, amesema kwa mwaka jana tani 4500 za mbolea hiyo ziliuzwa na mwaka 2023/24  serikali imeitengea kampuni hiyo Sh.Bilioni 40 ili kuingia kwenye ushindani wa kununua mbolea ya ruzuku kwa ajili ya wakulima.

“Tayari kampuni imeagiza mzigo kutoka nje ya nchi na tunatarajia kupokea wiki ya kwanza hadi ya tatu ya mwezi Julai mwaka huu mbolea ya kupandia na kukuzia tani 25,000,”amesema.

Amesema wameingia makubaliano na vyama vikuu vya ushirika takribani 20 ili kuwauzia mbolea wanachama.

About the author

mzalendoeditor