Featured Kitaifa

UFUNGUZI WA MAFUNZO KWA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MTAA, WATENDAJI WA KATA KATIKA ZOEZI LA UHAKIKI WA ANWANI ZA MAKAZI.

Written by mzalendoeditor
Na. Mwandishi Wetu
 
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari leo Juni 19, 2023 imefungua rasmi mafunzo ya siku tatu kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Watendaji wa Kata na Mitaa, katika zoezi la Uhakiki wa Anwani za Makazi Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Ukumbi wa La Dariot, Mkoa wa Dar es salaam.
 
Akifungua mafunzo ya zoezi hili Ndgu Saloni Nyika, akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam (RAS), amewasihi washiriki wa zoezi hilo wakashirikiane na wajumbe wao huko waendako ili kulifanya zoezi hilo kuwa rahisi na linalohamasisha wengine kuendelea na uhakiki.
 
“Wenyeviti wa serikali za mitaa, niwaombe mkashirikiane na wajumbe wenu kuhamasisha wananchi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi” alisihi Bw. Nyika.
 
Aidha, Bw. Nyika alisisitiza kuwa zoezi hili lihamasishe wananchi kutunza, kulinda vibao vya namba za nyumba na miundombinu yote ya Anwani za Makazi kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania wote.
 
Kwa upande wake Ndgu Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habbari amesema Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inadhamira ya kuboresha Mitaa na mazingira yote Tanzania isomeke kwa anwani za makazi kama zilivyo nchi zingine zilizoendelea.
 
Mafunzo hayo yanafanyika kwa nia ya kuhakiki, kurekebisha na kusasisha taarifa zote zilizopo uwandani ili kuboresha zoezi kwa matumizi sahihi ya anwani hizo za makazi ambapo zoezi hili ni la nchi nzima.
 

About the author

mzalendoeditor