Jeneza lililobeba mwili wa Mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu John Samuel Malecela, Marehemu William Malecela maarufu kwa jina la Lemutuz wakati wa maombolezi na kuaga mwili wake katika Viwanja vya Karimjee leo Mei 15,2023 Jijini Dar es Salaam.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe.Omary Kumbilamoto akizungumza na waombolezaji wa msiba wa Mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu John Samuel Malecela, Marehemu William Malecela maarufu kwa jina la Lemutuz katika Viwanja vya Karimjee leo Mei 15,2023 Jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba akizungumza na waombolezaji wa msiba wa Mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu John Samuel Malecela, Marehemu William Malecela maarufu kwa jina la Lemutuz katika Viwanja vya Karimjee leo Mei 15,2023 Jijini Dar es Salaam
Samuel John Malecela ambaye ni mdogo wake na marehemu William Malecela maarufu kwa jina la Lemutuz akizungumza wakati wa maombolezi na kuaga mwili wake katika Viwanja vya Karimjee leo Mei 15,2023 Jijini Dar es Salaam.
Gari lililobeba mwili wa Mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu John Samuel Malecela, Marehemu William Malecela maarufu kwa jina la Lemutuz wakati wa maombolezi na kuaga mwili wake katika Viwanja vya Karimjee leo Mei 15,2023 Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa ndege aina ya Bombadier kwa ajili ya kuusafirisha mwili wa Mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu John Samuel Malecela, William Malecela maarufu kwa jina la Lemutuz
Akizungumza Mei 15, 2023 mbele ya waombolezaji waliojitokeza kumuaga mwili wa marehenu Lemutuz katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaaam, Mshereheshaji wa shughuli hiyo(MC) Hajji Manara amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia imetoa ndege kuusafirisha mwili wa Lemutuz.
Amesema ndege ambayo imetolewa na Serikali ina uwezo wa kubeba abiria 70 na kitendo cha Serikali ya Rais Samia kutoa ndege hiyo inaonesha inatambua mchango wake ambao ameutoa kwa jamii ya Watanzania.
“Tunampongeza Rais wetu Mama Samka Suluhu Hassan kwa kutoa ndege aina ya Bombadier kuusafirisha mwili wa Lemutuz, tunafahamu Lemutuz licha ya kuwa ni mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu mzee John Malecela lakini inaonesha kuwa Serikali inathamini mchango wa Lemutuz katika kutoa mchango wake kwa jamii, ” amesema Manara.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Dar es Salaam amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa usafiri wa ndege kumsafirisha Lumetuz.”Tunamshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuonesha utu wake kwa Watanzania, tunamshukuru kwa kutoa usafiri kumsafirisha ndugu yetu Lemutuz.”
Akimzungumzia Lemutuz amesema alikuwa ni mtetezi mkubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia alikuwa akiwatetea hata watu binafsi kwenye mitandao ya kijamii na hakika vijana wanapaswa kuendelea pale ambapo Lemutuz ameishia.
Mbunge wa Jimbo la Ukonga ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuikimbilia familia ya Waziri Mkuu mstaafu Malecela kwa kuamua kutoa usafiri wa ndege kuusafirisha mwili wa Lemutuz .
Ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba Lemutuz alikuwa mtu mkweli na aliamini katika ukweli hata kwa wale marafiki zake “Kuna rafiki yetu mmoja aliomba ushauri kwa William lakini akamwambia hawezi kumsadia na hataki kuwa mnafiki, hivyo unaweza kuona Lemutuz alikuwa anasimama kwenye ukweli na hakuwa mnafiki.”
Wakati huo huo kaka wa William Malecela, Samuel Malecela ametoa wasifu mfupi wa marehemu, ambapo amesema amezaliwa Machi 25, 1961/katika kijiji cha Mvumi mkoani Dodoma.
Amesema alipata elimu yake ya msingi Mvumi na baadae alijiunga na Shule ya Sekondari ya Mazengo na alipomaliza elimu ya sekondari alienda nchini Marekani ambapo alipata Shahada mbili na kisha kuamua kuishi huko.
Amesema Willima (Lemutuz) ameacha watoto wawili wanaoishi Marekani na kwamba alirejea nchini miaka ya 2000 na kuamua kuanzisha mtandao wa kijamii unaojulikana Lemutuz.
Kuhusu changamoto ya ugongwa, Samuel amesema kwamba alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo na mara kwa mara alikuwa anaenda nchini India kwa matibabu lakini pia alikuwa akipata matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI).
“Alipatwa na tatizo ghafla na kukimbizwa Hospitali ya Mnazi mmoja kwa ajili ya matibabu lakini baada ya vipimo ilibainika kuwa tayari ameaga dunia, ” amesema Samuel na kuongeza wanaishukuru Serikali kwani kuanzia Serikali ya Awamu ya Tano lakini pia na Awamu ya Sita imekuwa imesaidia matibabu yake mara kadhaa.