Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Bi.Marry Chatanda,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Mei 12,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya kusikitishwa na Kitendo cha Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA) kutumia mabango kwenye maandamano yao yenye lugha ya kejeli dhidi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Na.Alex Sonna-DODOMA
UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) umekemea kitendo cha Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA) kwa kutoheshimu mamlaka na kutumia lugha ya kejeli dhidi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo ni kinyume cha mila na desturi za kuheshimu viongozi wakuu wa nchini.
Hayo yamesemwa leo Mei 12,2023 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Bi.Marry Chatanda,wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa maandamano yaliyofanywa na BAWACHA Mei 11 mwaka huu wanachama hao walibeba mabango na kutoa kauli ambazo ziliomuhusisha moja kwa moja Rais Dk. Samia ambazo zilikuwa sio za kiungwana na zenye kebehi kwa kiongozi wa nchi.
Umoja huo umesema kuwa hautovumilia kauli hizo na utasimama imara kudumisha misingi ya kuheshimiana hususan wakati huu ambao Rais Dk. Samia amekuwa mstari wa mbele katika kujenga demokrasia imara na utawala wa sheria.
“UWT inaheshimu maridhiano ya kisiasa yaliyofanyika mpaka sasa na uhuru wa kuendesha shughuli za kisiasa na uhuru wa kuendesha shughuli mbalimbali za kisiasa na uhuru wa kujieleza ambao unalindwa nani ya katiba.
Ameongeza kuwa: “UWT haitokuwa tayari kuvumilia uhuru huo kutumika vibaya mfano lugha ya matusi, udhalilishaji na wenye kutweza utu na hasa ukiwa unamlenga Rais Dk. Samia na mkuu wa muhimili wa Bunge, Spika Dk. Tulia Ackson.”ameeleza Bi.Chatanda
Hata hivyo amefafanua kuwa katika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani yaliyofanyika Machi tatu mwaka huu, BAWACHA ndio walimuhitaji Rais Dk. Samia kuhudhuria mkutano ulioandaliwa na chama hicho ambapo kwa ushupavu, rahimu, usikivu na ukarimu, Rais Dk. Samia alikubali mwaliko huo kwa dhamira ya kuliunganisha taifa.
Amesema kuwa katika maadhimisho hayo BAWACHA waliwasilisha ombi la kutaka wabunge wao 19 waondolewe Bungeni ambapo Rais Dk. Samia aliwaeleza kwamba jambo hilo lipo mahakamani hivyo uubiriwe uamuzi wa mahakama.
“Kitendo cha BAWACHA kutumia hoja kuwaondoa wabunge hao 19 Bungeni wakimuhusisha Rais Dk. Samia tena kwa kutumia lugha ya kejeli bila kuheshimu mamlaka yake na pia kutumia jina lake moja sio cha kiungwana na hakiendani na heshima aliyowapa ya kukubali mwaliko wao, mila na desturi zetu za kuheshimu viongozi wetu na hata wale waliotuzidi umri,” amesisitiza
Akizungumzia kuelekea maadhimisho ya siku ya Familia Kimataifa amesema UWT ngazi zote kuanzia Tawi, Kata, Wilaya, na Mkoa kufanya makongamano mbalimbali ya kuwaleta wanawake pamoja na kuelimisha kuhusu maadili na kupiga vita mmomonyoko wa maadili nchini.
“Pia tuhimize upendo ndani ya familia ili tuweze kujenga familia bora na kupunguza kabisa matukio ya ukatili ndani ya familia ikiwemo matukio ya mauaji tutakapojenga familia imara ndio taifa imara,”amesema Bi.Chatanda