Featured Kitaifa

VIPAUMBELE 10 VYA WIZARA YA VIWANDA,BIASHARA NA UWEKEZAJI MWAKA 2023-2024

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha Kwa Mwaka  2023/2024,  leo Mei 4,2023.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha Kwa Mwaka  2023/2024,  leo Mei 4,2023.

Naibu Waziri, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe,akijibu swali bungeni lililoulizwa wakati wa kikao cha bunge kinachoendelea jijini Dodoma  leo Mei 4,2023.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah,akimsikiliza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha Kwa Mwaka  2023/2024,  leo Mei 4,2023.

Sehemu ya Viongozi na Watumishi wa wizara hiyo wakimfuatalia Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji,(hayupo pichani) wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha Kwa Mwaka  2023/2024,  leo Mei 4,2023.

Na.Alex Sonna-DODOMA

WIZARA ya Viwanda Biashara na Uwekezaji imetaja vipaumbele vyake  10 katika mwaka wa fedha 2023-204 ikiwemo kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Hayo yameelezwa leo,Mei 4,2023 Jijini Dodoma  na Waziri wa Wizara hiyo,Dk.Ashatu Kijaji wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo bungeni kwa mwaka wa fedha 2023-2024.

Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa  zaidi ya Sh bilioni 119 ambapo zaidi ya  Sh bilioni 75 ni kwa matumizi ya kawaida na zaidi ya Sh bilioni 63 ni mishahara na zaidi ya  Sh bilioni 43  ni kwa ajili ya  matumizi ya maendeleo.

Dk Kijaji amevitaja vipaumbele vya wizara hiyo kuwa ni  kutekeleza miradi ya kielelezo ya Magadi Soda Engaruka, Makaa ya Mawe – Mchuchuma na Chuma – Liganga.

Pia, uwekezaji  katika maeneo maalum ya kiuchumi (SEZ) na kongani za viwanda ikiwa ni pamoja na Nala SEZ, Kwala SEZ, Mkulazi SEZ, eneo maalumu la uwekezaji Bagamoyo;

“Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Utoaji Huduma.Kuboresha Mazingira ya Biashara.Kukuza Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.Kukuza Sekta Binafsi.Kuratibu majadiliano ya biashara baina ya nchi na nchi, Kikanda na Kimataifa na Kuimarisha Huduma za Biashara na Masoko,”amesema Dk Kijaji.

MALENGO

Dk Kijaji amesema katika mwaka wa 2023/2024 Wizara imepanga kukamilisha Sera, Mikakati na Miongozo ya kuendeleza sekta ya Viwanda,kuboresha na kuongeza ustawi na tija ya viwanda nchini.

Pia,kuwa na takwimu, tathmini na taarifa zitakazowezesha kuendeleza sekta ya Viwanda,kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vipya na kongani za viwanda,kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kielelezo.

Vilevile,kufanya majadiliano na mwekezaji ili kusaini Mkataba wa ubia pamoja na kulipa leseni za uchimbaji wa Makaa ya Mawe Katewaka,kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia (Geological study) na kulipia leseni za uchimbaji katika Mradi wa Makaa ya Mawe Muhukuru.

“Kuendeleza kiwanda cha KMTC katika Mkoa wa Kilimanjaro,kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya msingi katika Kongani ya Viwanda – TAMCO,Kuendeleza Kiwanda cha TBPL na kuendelea kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa zinazozalishwa,”amesema Waziri huyo.

Ameyataja malengo mengine ni kukamilisha majadiliano na mwekezaji na kusaini mkataba wa ubia (JVA Agreement) na kulipia leseni za uchimbaji – Maganga Matitu.

“Kutafuta mwekezaji na Kufanya ukarabati wa majengo katika kiwanda cha Mang’ula,Kufanya maandalizi ya awali kwa mradi wa mafuta ya kula (preliminary preparation for establishment of edible oil) na kuendelea kufanya ukarabati wa majengo ya Nyanza Glass ili kuvutia wawekezaji wa viwanda,”amesema Dk Kijaji.

MAZINGIRA WEZESHI YA KUFANYA BIASHARA

Dk Kijaji amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara nchini ili kuvutia mitaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema katika kutekeleza azma hiyo, Wizara imeendelea kufanya mapitio ya Sera mbalimbali zinazosimamia Uwekezaji, Viwanda na Biashara nchini.

Amesema Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996, Sera ya Maendeleo ya Viwanda (1996- 2020) na Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (2003) ambapo amedai sera hizo ziko katika hatua ya ukusanyaji wa maoni ya wadau.

Aidha, Sera ya Taifa ya Biashara (2003) ipo katika ngazi ya maamuzi ya Serikali.

“Sera hizo zinafanyiwa mapitio ili ziendane na mazingira ya sasa ya uwekezaji na biashara ikiwa ni pamoja na kujumuisha vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka (2021/2022 – 2025/2026) na mabadiliko mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi na kiteknolojia,”amesema Waziri Kijaji.

MAENDELEO YA BIASHARA

Waziri Kijaji amesema Serikali imepanga katika maendeleo ya biashara ,kusimamia, kuratibu na kuboresha mazingira wezeshi ya kufanya biashara nchini,kuwaunganisha wazalishaji, wasindikaji na wafanyabiashara na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Pia,kufanya tafiti mbalimbali kuhusu upatikanaji wa masoko ya mazao na bidhaa,kupitia Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo ya mwaka 2008,kutayarisha viwango 640 vya kitaifa katika sekta/Nyanja mbalimbali.

“Kutoa leseni ya ubora kwa bidhaa 800 kutoka katika sekta Mbalimbali,kusajili majengo 12,000 ya maeneo ya uzalishaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa za chakula na vipodozi (food and cosmetic premises),”amesema Waziri huyo.

VIWANDA VIDOGOVIDOGO

Dk Kijaji amesema Wizara inaendelea kuhamasisha na kuelimisha wajasiriamali wadogo na wa kati kurasimisha biashara zao na kufanya shughuli zao katika maeneo rasmi ili kuwawezesha kutambulika na Serikali na taasisi mbalimbali zikiwemo taasisi za kifedha.

Amesema katika kurahisisha upatikanaji wa kanuni na taratibu mbalimbali za urasimishaji biashara na huduma mbalimbali, Wizara imeandaa rasimu ya Mwongozo wa urasimishaji biashara nchini.

“Jumla ya taasisi 78 zinazohusika na usajili, utoaji wa leseni na vibali mbalimbali vya kuanzisha na kuendesha biashara nchini zimehusishwa katika Mwongozo huo,”amesema Dk Kijaji

Aidha, kukamilika kwa Mwongozo huo kutasaidia kupunguza muda na gharama kwa wajasiriamali wadogo na wa kati pindi watakapohitaji kujua kanuni na taratibu mbalimbali za kurasimisha biashara.

SEKTA BINAFSI NA UMMA

Aidha amesema serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Dialogue – PPD) kupitia Mabaraza ya Biashara ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa kwa lengo la kutatua vikwazo na changamoto zinazokwamisha biashara na uwekezaji.

Amesema katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023, jumla ya mikutano 10 imefanyika katika ngazi ya mikoa.

Amesema matokeo ya vikao hivyo ni kuendeleza juhudi za makusudi za kuchochea ushiriki wa Sekta Binafsi katika kufanya maboresho muhimu ya Sera, Sheria, Miongozo na Kanuni mbalimbali zinazosimamia Sekta Binafsi.

MIRADI YA KIMKAKATI NA AJIRA 101,353

Katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023 miradi ya kimkakati na uwekezaji imezalisha ajira 101,353 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

“Ikilinganishwa na ajira 72,395 zilizozalishwa kwa mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 28.6. Kati ya hizo, ajira zilizozalishwa kwa wanawake ni 27,588 na wanaume 73,765,”amesema Waziri huyo.

Aidha, ajira 81,082 zilikuwa ni kwa vijana kati ya umri wa miaka 18 – 35 ambapo zaidi ya asilimia 78 wanafanya shughuli zenye ujuzi wa chini na asilimia 14 ni za ujuzi wa kati na asilimia 8 ujuzi wa juu.

Vile vile, miradi ilitoa fursa kwa watu wenye ulemavu 237 katika ajira za ujuzi wa kati na juu.

About the author

mzalendoeditor