Featured Kitaifa

KM 612.14 ZA BARABARA KUJENGWA MKOANI MOROGORO

Written by mzalendoeditor

Kazi zikiendelea za ujenzi wa mizani mpya ya kisasa itakayopima magari yakiwa kwenye mwendo (Weigh in Motion), katika mizani ya Mikumi iliyopo katika barabara kuu ya Morogoro – Iringa (TANZAM Highway), mkoani Morogoro.

Muonekano wa Sehemu ya barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9), inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Morogoro. Ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Eng. Lazeck Alinanuswe, akieleza kwa vyombo vya habari utekelezaji wa miradi ya ujenzi ya miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo.

Muonekano wa Daraja la Ruaha Mkuu ambalo ni sehemu ya barabara ya Kidatu hadi Ifakara (km 66.9) inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Morogoro ambao ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 78 na unagharimu kiasi cha Bil 105.

Imeelezwa kuwa kuanza  kutekelezwa kwa ujenzi wa barabara mpya zenye urefu wa kilometa 612.14 kwa kiwango cha lami mkoani Morogoro kutaufungua mkoa huo kwa kuunganisha halmashauri zake zote kwa lami. 

Hayo yamesema na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Eng. Lazeck Alinanuswe, wakati akieleza miradi ya kimkakati inayoendelea na ile inayotarajiwa kuanza kutekelezwa ambapo amefafanua kuwa miradi hiyo mipya zabuni zake zimetangazwa na iko katika hatua za mwisho ili kuweza kusainiwa ili kuanza utekelezaji. 

Ameitaja miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Ubena Zomozi – Ngerengere (Km 11.6), barabara ya Ifakara – Mbingu (km 62.5),  barabara ya Mbingu – Chita JKT (km 37.5), barabara ya Ifakara – Lupiro – Mahenge/ Lupiro – Malinyi- Kilosa kwa Mpepo- Londo – Lumecha na Malinyi JCT – Malinyi (km 422.54) na barabara ya Bigwa – Mvuha (km 78) pamoja na madaraja ya Ruvu na Mvuha. 

“Barabara hizi zote zikikamilika zitainua uchumi wa wananchi wa mkoa wa Morogoro pamoja na kuchochea maendeleo yake maana ni barabara za kimkakati”, amefafanua Eng. Lazeck. 

Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za ujenzi wa miundombinu hiyo kwa mkoa huo ambayo inatarajiwa kuanza mapema iwezekanavyo. 

Vilevile Eng. Lazeck ameeleza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara (km 66.9) kwa kiwango cha lami ambao umefikia asilimia 78 na unagharimu kiasi cha Bil 105. 

“Ujenzi wa Barabara ya Kidatu hadi Ifakara unakwenda vizuri na hadi sasa mkandarasi amekamilisha km 43 za lami na kazi nyingine zinaendelea kwa hatua nzuri na kwa upande wa madaraja yote yamekwishakamilika kwa asilimia 83 na Daraja la Ruaha Mkuu imebakia kuweka kitako cha juu ili kazi likamilike”, ameeleza Eng. Lazeck. 

Amefafanua ujenzi wa barabara na daraja hilo unatekelezwa na mkandarasi Reynolds Construction Company kutoka Nigeria na kusimamiwa na kitengo cha usimamizi wa miradi cha TANROADS (TECU) unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2023. 

Aidha, ameeleza kuwa Serikali imetoa fedha kiasi cha Bil. 1.9  kwa ajili ya utekelezaji wa maboresho ya mizani ya Mikumi katika barabara ya Morogoro-Iringa (TANZAM Highway) na Mizani ya Michese  katika barabara ya Dar es Salam-Morogoro kwa kuweka mizani ya kisasa inayopima magari yakiwa kwenye mwendo (Weigh in Motion) kwa lengo la kuzilinda barabara kwa kutoharibiwa na uzito mkubwa wa magari pamoja  na kupunguza msongamano wa magari katika maeneo hayo. 

Nao Wananchi wa Wilaya ya Ifakara wameishukuru Serikali kwani kukamilika kwa barabara ya Kidatu – Ifakara kumefungua fursa za kiuchumi Wilaya humo pamoja na mikoa ya jirani.

About the author

mzalendoeditor