Mradi wa afya ya macho katika mikoa ya Morogoro na Singida umeonyesha kuwa kuna uwezekano wa kuepuka upofu unao zuilika nchini Tanzania. Mnamo 2022, ilikadiriwa kuwa watu milioni 8.2 nchini walipoteza uoni na bila juhudi za makusudi, idadi hii inaweza kuongezeka (ripoti ya IAPB, 2020).
Boresha Macho, ni mradi wa afya ya macho uliosimamiwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sightsavers, uliolenga kurejesha na kulinda uoni kwa kutoa huduma ya afya macho kwa makundi yote yakiwemo, wazee, watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu.
Ukifadhiliwa na serikali ya Uingereza kupitia UK Aid Match na kutekelezwa na Sightsavers kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ya Tanzania, mpango huo ulisaidia zaidi ya watu 178,000 kupata huduma za msingi za afya ya macho. Aidha, mradi huo ulilenga hasa watu wenye ulemavu na wanawake, ambao kwa kawaida hukabiliwa na vikwazo vya kupata huduma za afya japokuwa hawapaswi kuachwa nyuma.
Mradi huo umebadilisha maisha ya watu kama Bibi Holo kutoka mkoani Singida ambaye anaweza kulima na kutunza wajukuu zake. Kupoteza uoni kutokana na mtoto wa jicho kulifanya kazi hizi kuwa ngumu na Holo alihisi kutokuwa na nguvu kwenye miguu yake.
Upasuaji wa mtoto wa jicho umempa “mwanzo mpya”. Anahisi furaha, nguvu, na anaweza kufanya kazi na kutembea tena. Holo sasa amemuhamasisha kaka yake pia kutafuta matibabu kwa tatizo lake la uoni.
Edwin Maleko, Meneja Programu wa Sightsavers, anasema: “Upatikanaji wa huduma za afya ya macho ni haki ya msingi ya binadamu na afya ya macho bora ni sawa na fursa, kuruhusu watoto kujifunza na watu wazima kufanya shughuli za kujipatia riziki.
Kuzingatia afya ya macho ni sehemu muhimu katika kuleta mwamko katika elimu, ustawi wa jamii, uchumi na matokeo ya afya bora. Ambayo hatimaye husaidia kupunguza umaskini na kutoa fursa kwa watu binafsi, jamii na taifa kustawi.”
Upatikanaji wa huduma ya macho uliboreshwa kupitia mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
• Upasuaji wa mtoto wa jicho kwa zaidi ya watu 17,000 na utoaji wa miwani kwa zaidi ya watu ,7000
• Uchunguzi katika jamii kwa njia ya huduma ya mkoba/kliniki tembezi. Mafunzo ya kitaalamu kwa wahudumu wa afya ya macho
• Ukaguzi na uboreshaji wa upatikanaji wa huduma katika vituo vya afya
• Mafunzo jumuishi ya ulemavu na ushirikishwaji wa kijinsia kwa wataalamu wa afya
•Kuongeza uelewa kwa kushirikiana na mashirika ya wanawake na watu wenye ulemavu.
Edwin anaendelea kwa kusema: “Tunaihimiza serikali na wadau wengine kuendelea kuboresha huduma za afya ya macho na mafunzo ya kitaaluma. Aidha, kujumuisha huduma ya macho katika mifumo ya elimu ili kukabiliana na afya ya macho ya mtoto, na kufanya kazi kwa karibu na mashirika ya wanawake na watu wenye ulemavu ili kuhakikisha huduma zinabaki kuwa jumuishi.
Mradi wa Boresha Macho uliwezekana kutokana na msaada mkubwa kutoka serikali ya Uingereza katika kampeni ya kuchangisha pesa ya Sightsavers ‘End is in Sight’. Ilianza kutumika kuanzia Oktoba 2019 mpaka Disemba 2022 na iliweka misingi imara ambayo serikali na washirika sasa wanaitumia. Bajeti za afya na rasilimali tayari zimeongezwa na Sightsavers kwa sasa inasaidia mapitio ya mitaala ya mafunzo ya kitaaluma.