Na. Asila Twaha – H/Mtama
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa imewaelekeza watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kusimamia fedha za Umma na kuhakikisha fedha inayotumika inaendana sambamba na ubora, thamani na uhalisia wa ujenzi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Halima Mdee(Mb) amesema kamati itaangalia usimamizi wa fedha za umma kama zimetumika kulingana na ubora na uhalisia wa uwekezaji uliofanyika.
Amesema hayo Machi 22, 2023 wakati Kamati ya LAAC ilipokagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama na kukuta kiasi cha fedha kilichotumika katika ujenzi hakiendani na ubora, muonekano na uhalisia wa majengo hayo.
Ameyataja majengo ambayo bado hayajakamilika kuwa ni jengo la watoto ambalo limefikia asilimia 76, jengo la wanawake asilimia 80 na wanaume kufika asilimia 40 na kueleza kuwa kiasi cha fedha kilichotumika ni kikubwa ikilinganishwa na uhalisia ulipofikia.
Awali ikisoma taarifa ya ujenzi wa Hospitali hiyo Kaimu Mkuu wa Idara ya Miundombinu Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Bw. Abruhani Juma amesema mpaka sasa majengo hayo matatu walishapokea Tsh. milioni 500.
Amefafanua kuwa changamoto ya kutokukamilika kwa majengo hayo matatu ni kutokana na mabadiliko ya bei ya vifaa katika soko na hivyo huathiri maelekezo na malengo ya utekelezaji wa mradi uliokusudiwa.
Pia kamati imeitaka Wizara ya TAMISEMI kuona umuhimu wa kuajiri wahandisi ili waweze kusimamia miradi mikubwa kuendana na thamani ya fedha inayotolewa na Serikali.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Charles Mahera ameishukuru kamati kwa kuendelea kusimamia fedha za umma na kuahidi kuendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha fedha zote zinazopelekewa katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinasimamiwa kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taribu ili lengo la ujenzi wa miradi kwa ajili ya utoaji wa huduma kwa wananchi ufikie malengo.
“Mkoani walishapatiwa Mhandisi na amesharipoti ni vizuri kumtumia” Dkt. Charles